Na John Walter-Manyara
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa
Manyara, Wenceslaus Ignace Mtui, amekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa watendaji wa
idara za ardhi katika halmashauri tano za mkoa huo, ikiwa ni jitihada za
kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akikabidhi vifaa hivyo, Mtui amesema
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa msaada huo kwa lengo la kusaidia
upatikanaji wa huduma za ardhi kwa haraka na kwa ufanisi katika halmashauri
zote za Mkoa wa Manyara.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha
wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati, hususan katika masuala ya
umilikishaji na usimamizi wa ardhi.
Aidha, Mtui ametoa rai kwa watendaji wa
ardhi waliokabidhiwa vifaa hivyo kuhakikisha wanavitumia kwa malengo
yaliyokusudiwa na kuvitunza ipasavyo.
Amewasisitiza kufanya kazi kwa weledi na
ufanisi ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi, hususan migogoro ya
ardhi ambayo imekuwa ikiathiri maendeleo katika baadhi ya maeneo.
“Ni muhimu kuhakikisha migogoro ya ardhi
inamalizika katika maeneo yenu, wananchi wanapatiwa hati zao kwa wakati, na
makusanyo ya kodi ya ardhi yanafanyika ipasavyo ili fedha hizo ziweze kutumika
kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi wengine,” amesisitiza Mtui.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kila
halmashauri imepatiwa kompyuta mbili, UPS mbili pamoja na printa moja.
Vifaa hivyo vinatarajiwa kuongeza
ufanisi katika utunzaji wa kumbukumbu, uchakataji wa nyaraka na utoaji wa hati
za ardhi.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya
mkakati mpana wa serikali wa kuimarisha sekta ya ardhi na kuhakikisha wananchi
wanapata huduma stahiki kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
0 Maoni