Na John Walter-Babati
Tukio la kusikitisha limeutikisa wakazi wa eneo la Magugu, wilayani Babati mkoani Manyara, baada ya mwili wa mwanaume ambaye bado hajatambulika kukutwa umetupwa pembeni mwa barabara kuu ya Babati–Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, marehemu ana dalili za
kuuawa kikatili, huku chanzo cha tukio hilo kikiwa bado hakijabainika.
Wananchi wa eneo hilo wameeleza hofu kubwa kufuatia tukio
hilo, wakihofia usalama wao na kuziomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka
kuwabaini wahusika na kuimarisha ulinzi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Magugu, Lohay Amos, amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo, akieleza kuwa limetokea usiku wa kuamkia Machi 19
katika eneo la Kwa Chami.
Amesema mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa na majeraha makubwa
kichwani, ambapo inaelezwa kuwa alipigwa na kitu kizito kinachofanana na shoka,
hali iliyosababisha kuharibika kwa taswira ya uso na kufanya kuwa vigumu
kutambulika.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia
maiti katika Kituo cha Afya Magugu huku uchunguzi ukiendelea.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Babati, Mrakibu wa Polisi Ernesta
Mwambinga, alifika eneo la tukio na kuwahakikishia wananchi kuwa Jeshi la
Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo
la kinyama.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa
zozote zitakazosaidia uchunguzi, akisisitiza kuwa taarifa hizo zitahifadhiwa
kwa siri.
Wananchi wa Magugu wamelalamikia kuongezeka kwa matukio ya
ukatili katika eneo hilo, wakitaka ulinzi uimarishwe pamoja na uwekaji wa taa
za barabarani, hasa katika maeneo yenye giza nene nyakati za usiku.
Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kumtambua
marehemu na kubaini ukweli wa tukio hilo.
0 Maoni