Na John Walter-Babati
Vijana katika Kata ya Magugu, Halmashauri ya Wilaya ya
Babati, wamekabidhiwa pikipiki nane zenye thamani ya shilingi milioni 24,
zikiwa zimewekewa bima na kusajiliwa LATRA, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa
mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri inayolenga kuwawezesha wananchi
kiuchumi.
Akikabidhi pikipiki hizo Februari 12, 2026 katika mkutano wa
hadhara uliofanyika Kijiji cha Magugu, Diwani wa Kata ya Magugu, Stanley
Charles, amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatamani kuona wananchi wanainuka
kiuchumi, ndiyo maana Serikali inaendelea kusisitiza uwezeshaji wa vijana,
wanawake na watu wenye ulemavu kupitia mikopo hiyo isiyo na riba.
Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Babati imekuwa ikitekeleza
kikamilifu maelekezo hayo kwa kuhakikisha makundi mbalimbali yanapata mikopo ya
kuwawezesha kujiajiri na kuboresha maisha yao.
Aidha, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kusimamia
vyema upatikanaji wa fedha za mikopo hiyo, akisema hatua hiyo ni chachu ya
kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa
Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Januari Bikuba, amesema Serikali ina nia ya
dhati ya kuwainua wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa
kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, na kuwataka wananchi
kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kutumia vyema fursa zinazotolewa.
Bikuba amebainisha kuwa hadi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Babati imeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 tangu Serikali iruhusu kuendelea kwa utolewaji wa mikopo hiyo.
Ameeleza kuwa mikopo hiyo
hutolewa kwa vikundi vilivyosajiliwa vinavyojipambanua juu ya shughuli za
kiuchumi wanazokusudia kufanya.
Aidha, amewasisitiza wanavikundi kuhakikisha wanatumia
mikopo hiyo kama ilivyokusudiwa na kurejesha kwa wakati uliopangwa ili kutoa
nafasi kwa wengine kunufaika na mpango huo.
0 Maoni