Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimeadhimisha Siku ya Ukombozi ya Kusini mwa Afrika kwa shughuli mbalimbali jijini Harare, zikiwa na lengo la kuenzi historia ya harakati za ukombozi na kuhamasisha uhifadhi wa urithi wa kihistoria.
Katika hafla hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda, aliwasilisha salamu kwa niaba ya Mheshimiwa Sarah Molosiwa, Mkuu wa Kundi la Mabalozi na Balozi wa Jamhuri ya Botswana nchini Zimbabwe, ambaye hakuweza kuhudhuria kutokana na majukumu mengine ya kikazi.
CP Kaganda, akiwakilisha hotuba ya Mheshimiwa Molossiwa, alisema kuwa hafla hiyo inawakumbusha wananchi juu ya ujasiri na kujitolea kwa wanaume na wanawake wengi waliopambana dhidi ya ukoloni, ukandamizaji na dhuluma. Aidha, aliongeza kuwa siku hii si tu kumbukumbu ya yaliyopita, bali pia ni wito wa kuendeleza maadili na misingi ya uhuru, mshikamano, na haki kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Maadhimisho hayo, yaliyoandaliwa kuanzia Machi 23 hadi 25, yalihusisha viongozi wa serikali, wanahistoria, na vijana kutoka mataifa mbalimbali ya ukanda wa SADC.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, alikuwa Mheshimiwa .Prof. Amon Murwira, Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe ambapo alisisitiza umuhimu wa umoja, mshikamano, na kuenzi historia ya ukombozi wa Kusini mwa Afrika.
Aidha, maadhimisho hayo yalitanguliwa na upandaji miti katika eneo la Heritage Village, tukio lililolenga kuenzi utamaduni na urithi wa kihistoria.
Siku ya Ukombozi ya Kusini mwa Afrika huadhimishwa kila mwaka tarehe 23 Machi, ikiwa na lengo la kukumbuka mchango wa harakati za ukombozi zilizowezesha nchi nyingi za ukanda huo kupata uhuru.

0 Maoni