F Madunga yang'ara kielimu;' Sala, Kula na Kusoma Vyaweka msingi wa Ufaulu. | Muungwana BLOG

Madunga yang'ara kielimu;' Sala, Kula na Kusoma Vyaweka msingi wa Ufaulu.


Na John Walter-Manyara

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati na Diwani wa Kata ya Madunga, John Noya, amesema katika kata hiyo wanafunzi wanapaswa kuzingatia mambo matatu muhimu ambayo ni kusali, kula na kusoma ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika mitihani ya taifa.

Noya ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea Shule za Sekondari Utwari, Madunga Girls na Umagi, ambako alizungumza na wanafunzi pamoja na walimu na kuwapongeza kwa matokeo mazuri ya kitaaluma.

Ziara hiyo pia ilikuwa ni sehemu ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa diwani wa kata hiyo.

Amesema baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Babati limeweka utaratibu wa kutambua kata zinazofanya vizuri katika mitihani ya taifa kwa kuzipongeza hadharani, huku zile zinazofanya vibaya zikikumbushwa wajibu wao mbele ya jamii ili kuongeza uwajibikaji katika sekta ya elimu.

“Nataka ufaulu uongezeke zaidi. Sitaki kuchekwa wala kuzomewa. Ndiyo maana kwenye baraza letu la madiwani tumekubaliana kuwa kata zinazofanya vizuri zinapongezwa mbele ya watu, na zile zinazofanya vibaya zinaitwa pia ili kujitathmini,” alisema Noya.

Amewapongeza walimu, wanafunzi pamoja na wazazi wa Kata ya Madunga kwa juhudi zao ambazo zimeiwezesha kata hiyo kufanya vizuri kitaaluma na kuiheshimisha wilaya na mkoa kwa ujumla.

Amewataka kuendelea kuongeza bidii ili kudumisha mafanikio hayo.

Aidha, Noya ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Manyara, aliwahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii huku akiwataka walimu kuendelea kutimiza wajibu wao kwa weledi ili kuinua zaidi kiwango cha elimu.

Katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika elimu, aliahidi kusaidia upatikanaji wa kompyuta katika shule hizo ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza masomo ya TEHAMA kwa ufanisi zaidi.

Kwa mujibu wa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2025 katika Mkoa wa Manyara, Sanu Seminary ilishika nafasi ya kwanza huku Shule ya Sekondari ya Wasichana Madunga inayomilikiwa na Jimbo Katoliki la Mbulu ikishika nafasi ya pili kimkoa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Madunga, Sr. Devota Maria Sabs, amempongeza Diwani Noya kwa juhudi zake za kuhamasisha maendeleo ya elimu katika kata hiyo na kuahidi kuwa shule hiyo itaendelea kufanya vizuri zaidi katika matokeo ya kitaaluma.

 


Chapisha Maoni

0 Maoni