Na John Walter-Manyara
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Manyara kimesema kiko bega kwa bega na serikali kuhakikisha kinakomesha migogoro ya ardhi inayozidi kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Akizungumza Aprili 11, 2026, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Manyara kilichofanyika kwenye ukumbi mdogo uliopo katika ofisi za CCM mkoa, Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Peter Toima, amesema chama kimejipanga kuchukua hatua madhubuti kudhibiti na kumaliza migogoro hiyo.
Ameeleza kuwa vikao halali pekee ndivyo vyenye mamlaka ya kufanya maamuzi ya mwisho kuhusu masuala ya ardhi, huku akisisitiza kuwa wenyeviti wa vijiji wanapaswa kuwa na mihuri rasmi ili kuhakikisha uwajibikaji na uhalali wa maamuzi yao.
Aidha, ameonya kuwa wenyeviti na madiwani wanaotokana na CCM wanapaswa kuepuka kujihusisha na migogoro ya ardhi, akisisitiza kuwa chama hakitasita kuwachukulia hatua wale watakaobainika kuchochea au kushiriki migogoro hiyo.
“Hatutamvumilia kiongozi yeyote, iwe ni wa serikali au wa chama, atakayebainika kusababisha migogoro ya ardhi. Chama hakitamtetea mtu wa aina hiyo, bali kitahakikisha anawajibishwa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Toima amegusia changamoto ya kilimo cha milimani kinachosababisha mmomonyoko wa ardhi, akitolea mfano maeneo ya Mbulu na Magara, pamoja na tatizo la ukataji miti ovyo unaochangia uharibifu wa mazingira.
Amesisitiza umuhimu wa matumizi bora ya ardhi na kuitaka jamii kushirikiana na viongozi kuhakikisha rasilimali hiyo inatumika kwa uangalifu ili kuepusha migogoro na kulinda mazingira.
CCM Manyara imeahidi kuendelea kusimamia nidhamu kwa viongozi wake na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wote watakaokiuka maadili ya uongozi katika suala la ardhi.

0 Maoni