📍Wanging’ombe,Njombe
Wakala ya Nishati Vijijini (REA) umeshiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 Wilaya ya Wanging’ombe mkoa wa Njombe, na kusambaza na kuuza mitungi ya gesi ya kilo sita kwa wananchi kwa bei ya ruzuku ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la REA kwenye maonyesho yaliyokuwa uwanja wa shule ya msingi Igagala,Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, ameipongeza REA kwa juhudi inayoendelea kuzifanya kutekeleza miradi ya nishati safi ya kupikia nchini kwa kuwa imekuwa na mchango mkubwa kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira.
Ameeleza kuwa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ni hatua muhimu katika kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira pamoja na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamekuwa yakichangia uharibifu wa mazingira kwa kiwango kikubwa.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi wa Wilaya ya Wanging’ombe kutumia fursa hiyo ya upatikanaji wa mitungi ya gesi kwa bei nafuu kubadilisha mtazamo na mfumo wa maisha yao kwa kuachana na matumizi ya nishati zisizo salama na kuanza kutumia nishati safi kama gesi, majiko banifu pamoja na nishati nyingine mbadala.
Katika hatua nyingine, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwa kinara wa matumizi ya nishati safi si tu nchini Tanzania bali pia barani Afrika na duniani kwa ujumla kupitia sera na mipango mbalimbali inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi kwa gharama nafuu.
Aidha, imeelezwa kuwa mitungi hiyo ya gesi kwa bei ya kawaida sokoni huuzwa kati ya shilingi elfu 40 hadi 50, lakini Serikali kupitia mpango wa ruzuku imetoa punguzo la asilimia 50 ili kuwawezesha wananchi hususan wa kipato cha chini kupata nishati hiyo kwa bei nafuu zaidi.
Kwa mujibu wa REA, jiko moja la gesi linauzwa kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500, huku mwananchi atakayehitaji kupata huduma hiyo akitakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA) kwa ajili ya usajili na uthibitisho wa mnufaika.




0 Maoni