Tanzania yashika nafasi ya tatu Afrika kwa wagonjwa wa Sikoseli huku mamia ya watoto wakichelewa kufikishwa hospitalini kutokana na imani za kishirikina.
Na John Walter
Watoto wenye Sikoseli wakipatiwa huduma hospitali. |
Watoto wengi wenye ugonjwa wa Sikoseli huchelewa kufikishwa hospitalini kutokana na imani potofu zinazohusisha ugonjwa huo na uchawi au laana.
Usiku mwingi wa utotoni kwake
ulikuwa wa vilio na maumivu makali ya viungo. Mara nyingine alikuwa akishindwa
hata kusimama. Macho yake yalibadilika na kuwa ya njano huku tumbo likianza
kuvimba taratibu.
Lakini kwa muda mrefu, familia
yake haikujua kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Sikoseli.
“Mara nyingi nilikesha nikilia
kwa maumivu. Wakati mwingine nilikuwa naishiwa damu kabisa,” anasimulia
mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 30 kutoka Manyara ambaye ameomba jina lake
lihifadhiwe kwa sababu za faragha.
Sauti yake upande wa pili wa simu
inaonesha historia ndefu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo ambao bado
umezungukwa na imani potofu katika jamii nyingi nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Mratibu wa huduma
za Sikoseli, Himofilia na magonjwa ya damu kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Asteria
Mpoto, jamii nyingi bado zinaamini kimakosa kuwa Sikoseli ni ugonjwa wa kulogwa
au laana.
“Jamii ielewe kuwa ugonjwa huu ni
wa kurithi kwa njia ya vinasaba. Sio wa kuambukiza wala sio wa kulogwa,”
anasisitiza Dkt. Mpoto.
![]() |
| Dkt. Asteria Mpoto kutoka Wizara ya Afya akisisitiza umuhimu wa jamii kuachana na imani potofu kuhusu ugonjwa wa Sikoseli. |
Takwimu zinaonyesha ukubwa wa tatizo hilo nchini Tanzania, zaidi ya watu laki mbili wanaishi na ugonjwa wa Sikoseli huku watoto wapatao 14,000 wakizaliwa kila mwaka wakiwa na ugonjwa huo.
Kwa Mkoa wa Manyara pekee,
wagonjwa 475 tayari wamebainika kuwa na Sikoseli.
Dkt. Mpoto anasema changamoto
kubwa si ugonjwa pekee, bali ni kuchelewa kwa wagonjwa kufikishwa hospitalini
kutokana na wazazi wengi kuamini ushirikina.
“Ukiona mtoto ana macho ya njano,
tumbo kuvimba au maumivu ya viungo, mpeleke hospitali haraka,” anasema.
Anasimulia tukio walilokutana
nalo katika ziara ya kitaalamu mkoani Singida.
“Tulikutana na mtoto amevimba
tumbo na amechanjwa sana tumboni. Tulipomuuliza mzazi alisema alianza kumpeleka
kwa waganga wa kienyeji.”
Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Dkt. Joshua Gideon, anasema wagonjwa wengi wanafika hospitali wakiwa tayari katika hali mbaya.
“Wengi wanaofika hospitali
unakuta tayari wamepitia kwa waganga wa kienyeji. Wanakuja wakati ugonjwa
umeshakomaa,” anasema.
Kwa sasa watoto 31 wenye Sikoseli
wanapatiwa huduma katika kliniki ya watoto ya hospitali hiyo huku idadi ya
wagonjwa ikiendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya,
ugonjwa wa Sikoseli unaweza kusababisha: Kuishiwa damu mara kwa mara, Kiharusi,
Matatizo ya figo, Matatizo ya moyo, Matatizo ya ini, Maumivu makali ya viungo.
![]() |
| Dkt. Joshua Gideon wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara akieleza changamoto ya wagonjwa wa Sikoseli kuchelewa kufikishwa hospitalini. |
Katika hatua ya kuleta matumaini kwa wagonjwa wa Sikoseli, serikali imefanikiwa kupunguza gharama za dawa za Hydroxyurea zinazosaidia kupunguza makali ya ugonjwa huo.
Dkt. Gideon anasema zamani dawa
hizo zilikuwa zikipatikana kwa gharama ya karibu shilingi laki mbili kwa mwezi
lakini sasa zinapatikana kwa takribani shilingi elfu ishirini kutokana na
jitihada za serikali.
“Hapo zamani dawa zilikuwa
zinapatikana kwa shida hata nje ya nchi, lakini sasa zinapatikana hapa nchini,”
anasema.
Wizara ya Afya pia imeendelea
kutoa elimu kupitia viongozi wa dini, waandishi wa habari pamoja na makundi
mbalimbali ya kijamii ili kuondoa dhana potofu zinazolizunguka ugonjwa huo.
![]() |
Dkt. Stella Malangahe wa Hospitali ya Benjamin Mkapa akieleza mafanikio ya huduma ya upandikizaji uloto kwa wagonjwa wa Sikoseli. |
Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma sasa imeanza kutoa huduma ya upandikizaji uloto kwa watoto wenye changamoto ya Sikoseli.
Daktari bingwa wa magonjwa ya
damu kutoka hospitali hiyo, Dkt. Stella Malangahe, anasema huduma hiyo imeanza
kuleta matumaini mapya kwa wagonjwa waliokuwa wakilazimika kutafuta matibabu
nje ya nchi.
“Mpaka sasa tumetoa huduma hiyo
kwa watoto takribani 30 na wanaendelea vizuri,” anasema.
Hata hivyo, anasema gharama za
huduma hiyo bado ni kubwa ambapo mgonjwa mmoja huhitaji takribani shilingi
milioni 75 kwa matibabu.
Kutokana na hali hiyo, hospitali
hiyo imeanzisha mfuko maalum wa matibabu ya upandikizaji uloto ikiwa ni sehemu
ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
Lengo ni kukusanya shilingi
bilioni saba kusaidia wagonjwa wengi zaidi kupata huduma hiyo.
“MAUMIVU YA SIKOSELI NAYAJUA…”
Baadhi ya
wanaoishi na Sikoseli wameendelea kuomba jamii kuachana na imani potofu na
kuamini tiba za hospitali.
Mwanamke huyo mwenye miaka 30
kutoka Manyara anasema maisha yake yamekuwa ya maumivu tangu utotoni.
Anasema hali hiyo ilimtesa hadi
alipofikisha miaka 20.
Kwa sasa ana familia, lakini
anasimulia kwa huzuni namna mtoto wake wa kwanza alivyofariki muda mfupi baada
ya kuzaliwa kutokana na Sikoseli kali.
Mtoto wake wa pili mwenye miaka
minne anaendelea vizuri baada ya kuzaliwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando
mkoani Mwanza na kufanyiwa vipimo mapema.
“nimeshuhudia Watoto wengi
wakipoteza maisha kwasababu ya wazazi wao waliwapeleka kwa waganga wa kienyeji
kwa kuamini Watoto wamelogwa”
“Kwenye hili kupata huduma tofauti na hospitali ni uongo kabisa. Wazazi waachane na imani potofu,” anasema.
Anaongeza kuwa kila anapoona
mtoto anaumwa huumia sana kwa sababu anayajua maumivu ya Sikoseli.
Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa
Manyara wameiomba serikali kuongeza elimu kuhusu ugonjwa huo.
Mkazi wa Manyara, Jaliwasson
Jasson, anasema jamii nyingi bado zinaamini ugonjwa huo ni laana.
“Elimu inahitajika sana ili
kuondoa imani hizi potofu,” anasema.
Kwa upande wake, Ruth Kyelula
anasema watu wengi wanaishi na changamoto hiyo bila kujua waanzie wapi kupata
msaada.
“Wananchi wanahitaji kuelekezwa
kuhusu huduma hizi,” anasema.
Tanzania inaendelea kupambana na
ugonjwa wa Sikoseli kupitia utoaji wa elimu, uchunguzi wa watoto wachanga na
kuhamasisha wananchi kupima vinasaba kabla ya ndoa au kuingia kwenye mahusiano.
Lakini wataalamu wanaamini vita
kubwa bado ipo kwenye kubadilisha mitazamo ya jamii.
Mtoto mwenye macho ya njano,
tumbo lililovimba au maumivu ya viungo hahitaji hirizi wala kuchanjwa tumboni.
Anahitaji vipimo, ushauri wa
kitaalamu na matibabu sahihi hospitalini.
Kwa sababu ukweli unabaki kuwa
mmoja: Sikoseli si uchawi, Sikoseli si laana.
Sikoseli ni ugonjwa na unatibika ukigundulika mapema.





0 Maoni