NA REBECA DUWE TANGA.
Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umefikia hatua muhimu ya utekelezaji, huku ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 86 na matarajio ya kukamilika ifikapo mwisho wa Agosti mwaka huu. Serikali imeeleza kuwa mafuta ya kwanza yanatarajiwa kupokelewa katika Kituo cha Chongoleani, mkoani Tanga, na kusafirishwa mwezi Januari 2027.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo la mradi Chongoleani, Waziri wa Nishati, Dkt. Deogratius Ndejembi, alisema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati unaounganisha Tanzania na Uganda.
Alisema kazi nyingi muhimu zimekamilika, huku kilichosalia kikiwa ni hatua za mwisho, ikiwemo kukamilisha miundombinu ya umeme itakayowezesha mitambo ya kusukuma mafuta kuanza kufanya kazi.
"Nimefurahishwa na maendeleo ya mradi. Kazi kubwa imefanyika na tunaamini ifikapo mwisho wa Agosti ujenzi utakuwa umekamilika. Ratiba inaonyesha kuwa meli ya kwanza itachukua mafuta ghafi kutoka Chongoleani mwezi Januari 2027," alisema Dkt. Ndejembi.
Serikali Yasisitiza Kukamilika kwa Miundombinu ya Umeme
Waziri Ndejembi alisema changamoto kubwa iliyobaki ni kukamilika kwa njia ya umeme kutoka Majani Mapana hadi eneo la mradi. Aliitaka Tanesco pamoja na mkandarasi anayetekeleza kazi hiyo kuhakikisha wanamaliza kwa wakati.
Alionya kuwa mkandarasi yeyote atakayeshindwa kutekeleza kazi hiyo kwa mujibu wa ratiba atachukuliwa hatua, ikiwemo kuondolewa kwenye orodha ya wakandarasi wanaofanya kazi na Tanesco.
Mradi wa Kipekee Afrika Mashariki
Kwa mujibu wa Waziri huyo, EACOP ni mradi wa kimkakati kwa Tanzania, Uganda na ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Alieleza kuwa bomba hilo lenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,400 ni la kwanza duniani kutumia mfumo wa kupashwa joto katika urefu wake wote.
Serikali ya Tanzania imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 973 kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ambalo linamiliki asilimia 15 ya hisa za mradi huo kwa kushirikiana na UNOC, TotalEnergies na CNOOC.
Ajira na Fursa kwa Watanzania
Dkt. Ndejembi alisema mradi umeendelea kutoa manufaa kwa Watanzania kupitia ajira na mafunzo ya kuongeza ujuzi.
Zaidi ya Watanzania 3,000 wamepata ajira za moja kwa moja kupitia mradi huo, huku zaidi ya vijana 100 wakipelekwa Madimba kwa mafunzo maalumu kabla ya kuajiriwa. Aidha, zaidi ya vijana 400 kutoka Chongoleani wamepatiwa mafunzo na kuajiriwa katika shughuli mbalimbali za mradi.
Tanga Yanufaika Kiuchumi
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, alisema mradi huo umeongeza shughuli za kiuchumi mkoani humo kupitia Bandari ya Tanga, ongezeko la mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na fursa za ajira kwa wananchi.
Alisema vifaa vingi vya mradi vimepitia Bandari ya Tanga kabla ya kusafirishwa katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji, hali iliyochangia kukuza uchumi wa mkoa.
Pia alibainisha kuwa mradi umezingatia viwango vya kimataifa vya utunzaji wa mazingira, huku shughuli za uvuvi zikiendelea bila kuathiriwa na ujenzi wa gati na miundombinu mingine.
Mbali na hilo, alisema jamii zinazozunguka eneo la mradi zimeendelea kunufaika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa mpira unaotumiwa na klabu ya Coastal Union.
Mradi Waingia Hatua za Mwisho
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa EACOP Tanzania, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Huduma za Mradi, Jofrey Mponda, alisema utekelezaji wa mradi umeingia katika hatua za mwisho, huku zaidi ya asilimia 90 ya kazi ikiwa imekamilika.
Alisema mradi unaounganisha mikoa 18 ya Tanzania na wilaya 27 umeanza hatua za ukaguzi na makabidhiano ya mifumo mbalimbali, ikiwemo vituo vya kusukuma mafuta, matenki ya kuhifadhi mafuta na miundombinu mingine muhimu.
Mponda alieleza kuwa pampu sita za kusukuma mafuta tayari zimejengwa, mbili zikiwa Uganda na nne Tanzania, huku pampu mbili za kupunguza shinikizo la mafuta zikiwa Chongoleani. Pia matenki manne ya kupokelea mafuta yamekamilika, na kazi iliyobaki ni kuunganisha mfumo wa umeme.
Aliongeza kuwa EACOP inaendelea kushirikiana na Tanesco kuhakikisha miundombinu ya umeme inakamilika ifikapo Septemba mwaka huu ili kuwezesha maandalizi ya kupokea mafuta ya kwanza mwezi Januari 2027.
Maendeleo ya mradi wa EACOP yanaonyesha kuwa Tanzania inaendelea kusogea hatua muhimu katika sekta ya mafuta na gesi. Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuongeza mapato ya serikali, kuchochea ukuaji wa uchumi, kuimarisha ajira na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji wa mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki



0 Maoni