BAADA YA SHERMAN, SAFARI YA COUTINHO YANUKIA KUTIMKA JANGWANI

Kumekuwa na uvumi kuwa, winga wa Yanga mbrazil Andrey Coutinho huenda akatimka kunako klabu ya hiyo na tayari kuna timu inamuwania ili kuinasa saini yake. Katibu mkuu wa Yanga Dkt. Jonas Tiboroha amesema , wao kama uongozi bado hawajapokea taarifa rasmi kutoka klabu  yoyote ikionesha nia ya kumtaka mchezaji huyo.

”Hatujapata document timu kutoka timu yoyote inayomtaka Coutinho kwenda kufanya majaribio au kumsajili jumla, lakini lisemwalo lipo bwana, huwezi kujua mara nyingi maajenti wanapitia kwa watu kabla ya kufika kwetu. Hata taarifa za Kpah Sherman zimekuja muda si mrefu lakini watu waliulizia kwa muda mrefu sana”, amesema Tiboroha.

Andrey Coutinho amekuwa akisugua benchi tangu alipopata majeraha ya muda mrefu kwenye msimu wa ligi uliomalizika na tangu arejee uwanjani amekuwa hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza.

Ujio wa Deus Kaseke kutoka Mbeya City pamoja na Godfrey Mwashiuya kutoka Kimondo umezidi kufuta ndoto za mbrazil huyo kuendelea kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Yanga kutokana na wawili hao kuonesha kiwango ambacho kimekuwa kikimvutia kocha mkuu wa timu hiyo Hans van Pluijm.


Coutinho alisajiwa Yanga na aliyekuwa kocha wa timu hiyo mbrazil Marcio Maximo na alionesha kiwango cha juu kwenye mechi zake za mwanzoni kabla ya kukubwa na majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu.