Ugonjwa hatari wa Ebola umeibuka tena nchini Sierra Leone
ambapo watu zaidi ya 500 wamekwenda kwenye karantini kaskazini mwa nchi hiyo,
baada ya mtu mmoja kuthibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano katika kituo cha taifa cha
kupambana na Ebola Sierra Leone ,
(NERC) Sidi Yayah Tunis
amesema maambukizi hayo yamefanya kijiji kimoja katika wilaya ya Tonkolili
kuwekwa kwenye karantini kwa siku 21.
Hassan Abdul Sesay, mbunge kutoka eneo hilo
amesema muathirika aliambukizwa Ebola katika mji mkuu, Freetown , na kwamba alikuwa amesafiri
kijijini kwa mnasaba wa sherehe za Idul Fitr.
Watu waliowekwa katika karantini ni pamoja na watumishi 30
wa hospitali iliyomhudumia mgonjwa ambaye baadaye alifariki dunia. Kwa mujibu
wa serikali ya Sierra Leone ,
taarifa za wagonjwa watatu zimeripotiwa ndani ya wiki mbili zilizopita.
Kwa mujibu wa takwimu za mwisho za Shirika la Afya Duniani
WHO tangu mwaka 2013 hadi sasa takribani
watu 26 elfu wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo huku wengine elfu 11 wakiwa tayari wamepoteza
maisha yao aghalabu wakiwa katika nchi za Sierra Leone, Liberia na Guinea
Conakry.