Mara nyingi sana katika
maisha yetu tumesikia maneno kama “nipe tano”
“chukua tano” maneno hayo yamekuwa maarufu na katika mazingira tofauti,
yamekuwa yakiashiria ushindi , au hali ya mafanikio au furaha baada ya hali
fulani.
Vivyo hivyo katika maisha yetu ya kutafuta kufanikiwa katika
yale yote tunayoyafanya kila siku viko vitu au hatua ambazo huwa zinatulazimu
kuzijua au kuzipitia kama kweli tunamaanisha
na tunadhamiria hayo mafanikio tunayoyatafuta.
Watu wengi hutamani mafanikio na kuyazungumzia sana katika maneno yao
ya kila siku lakini hawajawahi kuyaishi mafanikio hayo kwa sababu ya kutokuwa
na dhamira madhubuti katika kuyaelekea. Je, unajua ni hatua zipi muhimu za
kuelekea kwenye maisha ya mafaniko?
1.Kuwa na uwezo
binafsi wa kuvikagua vile ulivyo ndani yako.
katika maisha yetu ya kila siku hatuna budi namna ya
kujifunza kujikagua sisi wenyewe, kuvikagua vile tulivyonavyo ndani yetu kwa
sababu ni ukwelli kwamba pasipo kujikagua sisi wenyewe basi hatutaweza
kuyatambua mapungufu tulionayo na kama hatutoyatambua mapungufu hayo hayatoweza
kushughulikiwa na kuondelewa, maana yake ni kwamba tutazidi kushi na upungufu
wetu na hivyo kuathiri ufanisi wetu na mwisho wake mafanikio yetu kwa ujumla
yataathirika.
Labda nikupe mfano wa mtu mwenye duka , mara kwa mara huwa
na muda wa kuvikagua vitu au mali aliyo nayo dukani kwake na hapa huweza
kutambua nini kimepungua , nini hakipo kabisa na nini hakipo kwa wingi. Katika
kujikagua sisi wenyewe sio tu tutapata uhakika
wa vile tusivyonavyo bali pia tutapata kufahamu vile tulivyonavyo kwa
wingi. Jifunze kufanya tathmini ya maisha yako kila wakati, tathmini matendo
yako ya kila siku, maneno yako ya kila siku, mitazamo yako ya kila siku, halafu
angalia wapi kuna upungufu na wapi kuna fursa.
2. Uwezo wa kuwa na
msimamo.
Wengi wetu tumeshindwa kuyafikia malengo tuliyowahi
kujiwekea kwa sababu tu hatuna msimamo katika vile tunavyoviamini kwa hiyo
inakuwa ni rahisi kuyumbishwa na kupeperushwa na kila upepo unaokuja upande
wetu. Ili kufikia mafanikio tunayoyatamani
hatuna budi kuwa na misimamo fulani katika maisha. Naupenda msemo unaosema kama huwezi kuwa na msimamo na chochote basi utachukuliwa
na chochote.
Kama wewe ni kijana na huna msimamo katika baadhi ya mambo
basi ni rahisi kujikuta unabebwa na mengi kama
vile rushwa na ubadhilifu. Ni vyema kufahamu kila wakati maishani kuwa kama
huna msimamo katika ufanisi basi utaangukia katika uzembe na kutokuwajibika na kama hautakuwa na msimamo katika kuhakikisha unafanikiwa
basi utaangukia katika umaskini.
3. Uwezo wa kupiga
hatua.
Yamkini unatamani sana
kufanikiwa na kila siku unaongelea sana
mafanikio, ni vyema kujua kwamba mafanikio yetu hayaji kwa kuyatamani au
kuyaongelea bali katika uwezo binafsi wa kuamua kupiga hatua. Yawezekana upo
katika chombo kizuri tu cha usafiri lakini utajikuta unapitwa na kila mtu, hata
wale wenye vyombo vibovu vya usafiri nao watakupita kama
utakuwa umekaa tu kwenye chombo chako pasipo kuruhusu mwendo.
Chukua hatua kuelekea mustakabali wako, angalia mbele yako
unaona nini? Niniambacho unakiona kwenye mustakabali wako? Nini ungetamani ukipate kwenye mustakabali wako?
Anza kufanya kila kinachohusika ili kuona hiyo ndoto yako ikiwa dhahiri.
Anza kupiga hatua ya kwanza na hatua nyingine zitakuwa ni
rahisi kufuatia. Kamwe usitishike na umbali unaouona kuelekea mustakabali wako,
jinsi unavyopiga hatua ujasiri wako unafunguka na kukua, kumbuka kuwa kila
hatua unayoipiga hata kama ni ndogo kiasi gani
inakusogeza karibu na mustakabali wako.
4. Uwezo wa
kujitengenezea sura ya maisha yako.
Katika maisha yetu ya kila siku ni ama uamue kuitengeneza
sura ya maisha yako au kuibomoa sura hiyo, wengine wetu maisha yetu hayajawahi
kuwa na sura nzuri ya kuvutia.
Sisi wenyewe ndiyo wenye uwezo wa kuamua kuitengeneza sura
hiyo kuwa kama vile tunataka iwe, ukiamua
kukaa tu pasipo kufanya chochote basi umekusudia kwa dhamiri halisi kuiharibu
sura ya maisha yako mwenyewe.
Ulimwengu wa leo unabadilika kwa kasi sana , ili kuweza kubakia kwenye maana na
wenye umuhimu basi hatunabudi kuwezana na mabadiliko hayo. Kama
hutoweza kuyaweza mabadiliko ya karne hii basi mabadiliko hayo yatatuweza.
5. Uwezo wa kukikalia kiti na kuyaongoza
maisha yako mwenyewe.
Ziko nyakati ambazo wengi wetu hatuwezi kufika tunapotamani
kufika kwa sababu dereva anayeendesha chombo chako siyo wewe, wakati huohuo
unafikiria kuelekea pale unapopatamani wewe.
Ni ngumu katika maisha kama unaifahamu ndoto yako na unaiona
kesho yako na unaitamani sana
kuifikia basi amua kukaa kwenye kiti cha
dereva wewe mwenyewe na kuendesha chombo kuelekea huko.
Watu wengi siyo kwamba tumewakabidhi wengine udereva wa
safari yetu kwa kujua bali ni kwa kutokujua, mara unaona muelekeo wa safari
siyo ule unaoutarajia, yamkini sasa dereva uliyemkabidhi kiti anakupeleka
kwenye ndoto yake na siyo ya kwako tena.
Sasa amua kuingia kwenye kiti cha dereva wewe mwenyewe, hayo
ni maisha yako na siyo mwingine. Kamwe usiache furaha ya mafanikio yako katika
mikono ya mwingine. Kubali na kuwa tayari kubeba majukumu. Kama
unatokea unafanya makosa basi usijitetee na kukwepa, chukua tano!