Habari yako ndugu msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA
MAFANIKIO . Leo nataka tujikite kujadili ufugaji wa samaki na jinsi ambavyo
tunavyoweza kunufaika na ufugaji huu na kuweza hata kuongeza kipato chetu.
Kwanza kabisa samaki ni kitoweo kinachotumika na kupendwa
sana hapa nchini na duniani kwa ujumla, zaidi ya kupendwa tu ni kitoweo chenye
faida kubwa kwa mwili wa binadamu ambapo inaongeza protini ya kutosha na madini
na hivyo kuwa na mchango mkubwa kwenye mlo kamili.
Kwa hiyo basi kutokana na uhitaji mkubwa wa samaki, watu
wengi sasa wameamua kuanza ufugaji katika maeneo yao ,
na imekuwa biashara nzuri sana .
Ningependa basi kuwashirikisha katika mambo ya kitaalamu yanayotakiwa
kuzingatiwa katika ufugaji huu. Karibuni.
Ukitaka kuchimba
bwawa la samaki lazima kwanza uchague eneo linalofaa. Katika kuchagua eneo
linalofaa, kuna mambo ya kuzingatia kama
ifuatavyo;
i)
Eneo lenye vyanzo vya maji vya uhakika kama vijito, chemi chemi, na mifereji.
ii)
Eneo lenye mwinuko wa
wastani ili kurahisisha uchimbaji na uvunaji wa samaki kwa kukausha
bwawa.
iii)
Eneo lisilo na miti yenye kuleta kivuli.
.
iv)
Eneo lililo karibu na nyumbani ili iwe rahisi kuhudumia
bwawa na kuzuia maadui wa samaki
v)
Eneo lenye udongo unaofaa
.
Ninaposema udongo unaofaa ni ule wa mfinyanzi unaotuamisha
maji, kwa mfano udongo unaotumika kufyatulia tofali au kutengenezea vyungu.
Njia mbili hutumika kujaribu kama
udongo unafaa au la. Njia ya kwanza ni kuchukua udongo kwenye kiganja
kilichojaa, lowanisha na maji na kisha finyanga kama
tonge la ugali. Tupa juu tonge la udongo lililofinyangwa na lidake linaporudi
chini au liache lianguke chini.
Njia nyingine na ya uhakika zaidi ni ile ya kuchimba shimo
lenye kina cha kiuno. Jaribu udongo wa chini shimoni kama
ulivyofanya kwenye jaribio la kwanza. Kama tonge litatawanyika udongo huo
haufai na kama tonge litabaki limeshikamana,
endelea na jaribio lingine.
Mapema asubuhi jaza maji shimoni ili kuona kama
udongo utatuamisha maji. Finika shimo kwa kutumia matawi au kitu chocho ili
kizuia kuvukizwa ( evaporation). Jioni jaza tena maji iwapo yatakuwa yamenywea
ardhini.
Kama asubuhi inayofuata maji mengi yatakuwa yamebaki
shimoni, basi hilo
ni eneo zuri la kuchimba bwawa la samaki. Udongo huo utakuwa una uwezo wa
kutunza maji ya kutosha ambayo ni muhimu kwa samaki bwawani mwako.
Unaweza kuchimba bwawa lenye ukubwa wowote unaopenda.
Uchimbaji wa bwawa kubwa unahitaji muda, eneo, virutubisho na vilishio vingi
zaidi kuliko uchimbaji wa bwawa dogo. Hata hivyo utapata samaki wengi kutoka
kwenye bwawa kubwa.
Mfano bwawa lenye upana wa mita 10 na urefu mita 10 litakupa
samaki takribani 200. Bwawa lenye ukubwa wa mita 15 kwa 15 litakupa samaki kama 450 hivi.
Vitu vitakavyoamua ukubwa wa bwawa lako ni eneo ulilonalo,
upatikanaji wa mbolea ya kurutubisha maji na vyakula vya kulishia samaki. Ikiwa
huna mbolea na vyakula vya kutosha, ni bora kuchimba bwawa dogo.
Bwawa moja linalohudumiwa vizuri, litakupa mazao mengi zaidi
ya mabwawa mengi yenye huduma mbaya. Hivyo ni vema kuwa na bwawa moja
linalohudumiwa vizuri kuliko kuwa na mabwawa mengi yenye huduma duni.
Kumbuka kuwa Bwawa la samaki lina sehemu mbili kwa ndani,
sehemu yenye kina kirefu na sehemu yenye kina kifupi.
Itabidi pia ujenge sehemu ya kutunzia mbolea kwa kutumia
mianzi au miti kwenye moja ya kona upande wenye kina kirefu. Sehemu ya kutunzia
mbolea inatakiwa iwe na ukubwa wa asilimia 20 ya ukubwa wa bwawa lote.
Sehemu ya kutunzia mbolea itahifadhi mbolea ambayo utaweka
kwa ajili ya kurutubisha maji ya bwawa. Mbolea hii inatengeneza chakula cha
asili cha samaki.
Ukimaliza kuchimba bwawa, panda nyasi juu ya tuta kuzuia
mmomonyoko wa udongo inaoweza kuletwa na mvua. Baada ya yote hayo bwawa lako
liko tayari kujazwa maji, kurutubishwa kwa mbolea na hatimaye kupandikizwa
vifaranga vya samaki.
Katika makala ijayo Utapata maelezo zaidi ya jinsi
utakavyoweza kuwalisha samaki wako.
Endelea kufuatilia.