Israel Yatishia Kuishambulia Kijeshi Misri

Utawala wa Kizayuni wa Israel umetishia kuishambulia kijeshi Misri. Msemaji wa jeshi la Israel ametishia leo kuwa jeshi la utawala huo litalishambulia eneo la Sinai kwa kisingizio kuwa eneo hilo linahifadhi magaidi wenye silaha. Utawala wa Kizayuni unazishambulia nchi za eneo zikiwemo Lebanon na Misri kwa visingizio mbalimbali. Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel tayari limefanya maneva kubwa ya kijeshi ya siku tatu iliyokutanisha makumi ya maelfu ya vikosi vyake vya akiba huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Wakati huo huo ripoti kutoka katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zinasema kuwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameendelea kuwatia mbaroni raia wa Palestina huko Quds na katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Wanajeshi wa Israel leo asubuhi wameshambulia eneo moja huko Quds mashariki inayokaliwa kwa mabavu na kuwatia mbaroni Wapalestina kadhaa wakazi wa eneo hilo.

Kamatakamata hiyo ya wanajeshi wa Israel iliibua mapigano kati ya wanajeshi hao na vijana wa Kipalestina. Utawala wa Kizayuni unaendelea kuwatia mbaroni raia wa Palestina katika maeneo mbalimbali ya Quds na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, huku hadi sasa Wapalestina karibu elfu saba wakiwa katika jela za utawala huo dhalimu.