Jeshi la Kenya laua magaidi 3 wa Al-Shabab Lamu

Magaidi watatu wa kundi la kitakfiri la Al-Shabab wameuawa nchini Kenya katika Kaunti ya Lamu kufuatia mapigano na Jeshi la  Ulinzi la Kenya KDF.

Msemaji wa KDF Kanali David Obonyo amesema wanajeshi watano wamejeruhiwa katika mapigano hayo yaliyojiri karibu na eneo la Basuba, Lamu leo asubuhi saa nne.
Ameongeza kuwa wanajeshi wamefanikiwa kunasa bunduki mbili aina ya AK-47 na risasi kadhaa. Kanali Obonyo amesema gari la KDF lililengwa kwa bomu la kienyeji yapata kilomita saba kutoka Basuba na hapo wanajeshi waliokuwa wakilinda doria wakafyatuliana risasi na magaidi na kuwaua watatu kati yao.


Amesema magaidi kadhaa wakifanikiwa kutoroka wakiwa na majeraha. Wakaazi wa eneo hilo wamesema walisikia milio ya risasi na kuona moshi ukitoka katika Msitu wa Boni eneo ambalo jeshi la Kenya sasa linatekeleza oparesheni kali kuwatimua magaidi al-Shabab.