Kama Hujui, Mabilionea Wengi Duniani Wako Hivi

Kila kundi la kipato lina tabia na mienendo yake. Pengine kunakuwa na ugumu wa kuikwepa mienendo hiyo kwa wahusika, baada ya kuingia humo au mienendo hiyo ndiyo imewasaidia kufika hapo walipofika. Tunasema, kama alivyo binadamu ambapo kila mmoja ana haiba yake, makundi ya kipato nayo yana haiba zake, ambazo zinaweza kuwa tofauti na makundi mengine.

Kwa mfano, ukitazama kundi la mabilionea walio wengi duniani, utabaini kuwa wana sifa ambazo zinajitokeza sana kwa watu hao. Kuna sifa ambazo wanakuwa nazo na wala hawazipangi, bali ni kwa sababu ya mazingira au saikolojia ya fedha, wao wanakuwa na tabia au mienendo hiyo zaidi kuliko watu wa makundi mengine. Kutokana na mienendo hiyo mara nyingi ndiyo inawafanikisha sana.

Ukikagua sana, utakuja kugundua kuwa mabilionea walio  wengi ni wale ambao wanafanya biashara zinazohusiana na fedha, kama benki ikiwa pamoja na uwekezaji wa hisa, kuna ambao wanasughulikia mawasiliano kama simu na mitandao ya intaneti na hata kujishughulisha na ujenzi katika kiwango cha kimataifa au kwenye maeneo mbalimbali kama sehemu muhimu ya biashara zao.

Unaweza ukajiuliza maswali mengi kidogo na kuanza kushangaa biashara zingine vipi? haziwezi kumpa mtu utajiri na hatimaye kuwa bilionea? Siyo hivyo, kuwa kwamba biashara zingine haziwezi kumpa mtu ubilionea, hapana. Hizi ndizo ambazo zimewapa wengi ubilionea zaidi. Ukitazama kwa makini utagundua ukweli huu kuwa mabilionea wengi wamezalishwa kutokana na biashara hizo.

Pia mabilionea walio wengi wanatabia za kuacha mali zao kwa taasisi za kusaidia au hata kwenye nyumba za ibada au mifuko mbalimbali ya misaada baada ya kufa kwao.Na huacha fedha kidogo sana kwa watoto wao. Hapa kwetu, watoto wakishakuwa na baba mwenye fedha, hawataenda shule wala kujifunza maisha. Wanasubiri baba afe ili warithi. Wakati mwingine hurithishwa hata kabla baba hajafa. Matokeo yake ni kutapanya mali na kubaki mikono mitupu.

Hata kuna kipindi Bill Gates alishawahi kusema kwamba, hata iacha fedha yake kwa watoto wake, bali ataitumia kusaidia kuondoa matatizo yenye kusumbua sana dunia. Kabla hajafa ameshaanza kufanya hivyo. Watoto wake nao wanahangaika kivyao kujua maana ya kutafuta. Ni kwa sababu, kuwa sisi, ikiwemo kutafuta mafanikio kwa bidii zote, ndicho hasa kilichotuleta duniani. Hujaumbwa uwe maskini.

Lakini lingine la kushangaza zaidi ni kwamba, mabilionea wengi hawana hata digrii ya kwanza. Inawezekana walipitia vyuo lakini wakapata cheti au stashahada au walimaliza tu elimu ya msingi au sekondari. Kwa hiyo utakuja kugundua kuwa, fedha au utajiri hausiani sana na kusoma sana na hii inaonyesha haviko karibu. Mawazo, yaani unachoamini kuhusu fedha na utajiri, ndilo jambo la awali kabisa.

Mabilionea wengi pia hawakupewa urithi au kupata bahati nasibu katika maisha yao. Walio wengi  wametafuta fedha kwa juhudi zao wenyewe kwa kuanzia chini kabisa. Wengine waliweza kusota hadi wakawa kama vituko, lakini wakaja kusimama katika njia ambayo watu wengine wameshangaa na kubakia kusimulia wasielewe ni kitu gani kilichofanyika.

Kuna tatizo moja kwa mabilionea waliowengi. Kwa kufuata au kuhangaika kupata mafanikio zaidi, hujikuta wakisahau kwamba, kuna burudani, kuna ‘hobi’ na muda wa kusahau masuala ya shughuli. Wao ni watu wa kazi tu na ubunifu ndivyo vyenye kuwaumiza kichwa na si vinginevyo. Kuna wakati huwa wanajikuta hata wakipunguza hata masaa ya kulala sababu ya kufanya kazi kwa bidii zote.


Hebu jaribu basi kujikagua ili uone kama ni kweli nawe unaweza kuwa na sifa kadhaa kama hizo za mabilionea. Huenda nawe unatamani kuwa bilionea ila hujajua au kuamua ni kwa njia gani. Jua sifa zao, labda utawea kupima kiwango cha ukaribu wako kwao. Siyo lazima uwe na fedha nyingi ili kuwa bilionea, anzia hapo ulipo ukiwa umepania kuwa, unataka kuwa bilionea, utafanikiwa.