Shirika la ndege la Kenya Airways (KQ) limetangaza hasara
kubwa ya Shilingi bilioni 25.7 za Kenya sawa na dola milioni 257
katika kipindi cha fedha cha mwaka wa 2014-2015.
Hii ni hasara ya asilimia 661% ikilinganishwa na kipindi cha
fedha cha mwaka wa 2013-2014, Mwaka uliopita kampuni hiyo ya ndege ilitangaza
kuwa imepata hasara kubwa wakati huo ya shilingi bilioni 3.3 mwaka uliopita wa
kifedha.
Uongozi wa shirika hilo
unasema kuwa hasara hii kubwa imetokana na kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya Kenya , Shilingi ya Kenya imeporomoka kwa asilimia 11
ya thamani yake katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita miongoni mwa sababu
zingine.
''Ushindani kutoka kwa mashirika ya ndege kutoka ghuba na
mashariki ya kati, mbali na swala kuu la ugaidi imechangia pakubwa hasara kubwa
tuliyopata ''alisema Mkurugenzi mkuu mtendaji Mr. Mbuvi Ngunze.
Bwana Ngunze ambaye amechukua wadhfa huo mwezi Desemba mwaka
uliopita kutoka kwa mkurugenzi mkuu wa kipindi kirefu Dr. Titus Naikuni,
anasema kuwa Kenya Airways imekumbwa na msukosuko wa masoko yake kwani
yaliathirika na ugonjwa wa Ebola kwa kipindi kirefu cha mwaka uliopita, na
mfumuko wa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Habari hii sio nzuri kwa wenye hisa wakuu ambao ni Serikali
ya Kenya ambayo tayari, ilikuwa imeipa shirika hilo la KQ mkopo zaidi wa
shilingi bilioni 4.2 za Kenya ilikuisaidia kurejesha ushindani wake na
kuiwezesha kulipa mishahara wafanyikazi wake.
Kulingana na shirika hilo
kurejea kwao katika soko lake la Magharibi mwa Afrika kutaiwezesha kuleta faida
tena.
KQ vilevile iko mbioni kutafuta mkopo zaidi wa dola milioni
200m kutoka kwa benki ya Afrexim ilikuiwezesha kutekeleza wajibu wake kabla ya
kutathmini kima cha madeni yake.