Tunu muhimu za mafanikio ambazo Mungu amewekeza ndani ya
kila mtu ni vipawa/talanta. Kwa bahati mbaya sana na pengine kutokujua umuhimu wa vipawa,
watu wengi hawatilii maanani vipaji walivyonavyo. Wengi wanaishi kwa kuiga
maisha ya watu wengine kana kwamba wao ni nakala ya wengine. Kipaji chako ni
mtaji mkubwa kama utaamua kukitumia vizuri
ipasavyo. Kipaji chako ni fursa ya kufanikiwa maishani. Ni daraja la maendeleo
kwa binadamu yeyote yule.
Kipaji ni umahiri wa kipekee aliouweka Mungu ndani ya akili
ya mtu unaongoza usadifu wa viungo na fikra zake kufanya jambo Fulani kwa
upekee kabisa. Ni talanta ambazo mtu anazo siyo kwa sababu kasomea bali ni
ujuzi wa kuzaliwa nao, elimu inakusaidia tu katika kumfanya atumie kipaji chake
kwa ufanisi na kwa manufaa zaidi. Kwa mfano, michezo mbalimbali, sanaa kama mziki, kuchora, kucheza mpira, kuimba, kusanifu,
kubuni program za kompyuta, mitandao, na wakati mwingine kuchonga. Wapo watu
ambao wana vipaji katika eneo mojawapo wanachotakiwa kufanya ni kuvitumia
vipaji vyao.
Watu mashuhuri na wale waliofanikiwa sana ni wale waliotumia vipaji vyao vizuri.
Kuna mifano hai mingi kama Filbert Bayi wa Tanzania
alitumia talanta yake ya kukimbia mbio, wanamuziki kama
vile Michael Jackson, Rose Muhando walitumia sauti zao kufanikiwa. Na hata
wachezaji maarufu wanatumia vipaji vyao kucheza mipira na wanafanikiwa kuliko
hata wasomi wenye shahada lukuki.
Wasanii na wana michezo wengi ni miongoni mwa watu maarufu
na matajri sana duniani, japokuwa walio wengi
hawana elimu kubwa kiasi cha kushangaza , walichofanya ni kutumia vipawa vyao kama ipasavyo. Maana hata sukari iliyo katika chai bila
kukorogwa chai inaonekana haina sukari. Vivyo hivyo vipaji tunavyo, ili vifanye
kazi vizuri inabidi tuvikoroge.
Mungu alituumba na vipaji na talanta nyingi tofauti ili
tuvitumie kufanikiwa maishani. Kila mtu ana talanta yake imejificha ndani ya
umaizi wa akili yake. Tunahitaji kuweza kuziibua talanta hizo kule ziliko fichika, na kuzitumia huku tukibadili
mitazamo na kasumba. Huwa nasikitika sana
kumsikia mtanzania anasimama kwenye chombo cha habari akisema yeye ni maskini
anahitaji msaada. Wakati huo kafunika talanta zake kibindoni, na nyuma kaacha
ardhi kubwa, misitu mingi na hata watoto wengi ambao ni nguvu kazi muhimu
katika kuchangia maendeleo.
Wapo watanzania wanadiriki kusema kuwa “sisi tutaendelea
kubaki maskini hivihivi” na wengine wanadai umaskini wao ni mpango wa Mungu.
Huu ni uongo na ni dhambi. Mungu angetaka sisi tuwe maskini asingeweza kutupa
ardhi kubwa, asingetupa mvua nyingi na maji mengi, asingetupa samaki wengi,
asingetupa ndege na wanyama wengi wa mwituni. Asingutupa afya njema na nguvu.
Mungu alitupatia vyote hivi ili tuwe matajiri tuwasaidie na wale wanaoishi nchi
zisizo na ardhi (mawe tu), nchi zisizo na bahari, nchi zisizo na msitu, mto
wala bwawa. Sisi siyo maskini kamwe.
Na kiongozi au mwanasiasa anayetamka Tanzania ni
maskini(wakati yeye ni tajiri) huyo ni mpotoshaji. Tusiwafundishe watoto wetu
mtazamo hasi hata kama tunachangamoto. Kuwa na
matatizo ni sehemu ya changamoto za maisha, tunazipaswa kuzikabili. Maana
hakuna mtu au nchi inayojitosheleza. Ndio maana hata wao walioendelea huko
ulaya bado wanakuja kwetu kununua malighafi ili wakutumie huko kwao.
Tena nadhani hata walioita mkakati wa kukuza uchumi na
kupunguza umaskini(MKUKUTA) walikosea sana .
Ingefaa ukaitwa “mkakati wa kukuza uchumi na ustawi wa maisha ya watu”. Kuutaja
umaskini wakati tupo ndani ya utajiri mkubwa ni kujitafutia laana ya kudumu
.Maana kama tunakubali sisi ni maskini kamwe
hatuwezi kuweka mikakati ya maendeleo. Tunabaki na mikakati ya kimaskini.
Nafadhaishwa na mtazamo unaotaka kuzoeleka hapa Tanzania
miongoni mwa vijana kuwa mtu yeyote akifanikiwa: kumiliki nyumba nzuri, shamba
zuri lenye mavuno mengi, gari zuri, kiwanda na hata kuwa na elimu nzuri anaitwa
fisadi, yaani mwizi. Unakuta vijana wenye nguvu wanapita makazi ya watu wenye
nyumba nzuri wanasema “unayaona mahekalu ya mafisadi” wakimaanisha kuwa kila
nyumba nzuri, kiwanda kikubwa, shamba kubwa ni la fisadi au mwizi. Kwao
maendeleo ni wizi na siyo jitihada za kazi. Hawa wamepotoka sana .
Umaskini siyo mpango wa Mungu wala siyo ngozi ya kuzaliwa
nayo isiyobadilika. Hata vitabu vitakatifu kama
vile bibilia na msahafa vimesema wazi kwamba umaskini siyo mpango wa Mungu.
Mungu anataka kila mtu aishi maisha mazuri yenye ustawi huku akimpenda na kutii
mwongozo wake. Kila binadamu anahitaji maisha bora. Kila binadamu anahitaji
kulala pazuri, kula vizuri, kusafri vizuri, afya bora, kupata elimu bora,
mazingira safi ,
kucheza pazuri na kufurahia maisha kwa ujumla.
Watu wanakuwa kwenye shida kama
vile kuishi katika nyumba mbovu, na kula chakula kibaya au kisichotosheleza
siyo kwa sababu wao wanapenda, au kudhani kuwa maskini ndiyo sifa ya uadilifu.
La hasha ni kwa sababu hawana. Fikra za kuyaona maendeleo yoyote ya mtu au
kikundi cha watu ni ufisadi ni dalili kupoteza dira na kukosa matumaini
kuelekea ufukara wa kudumu na dhiki kuu.
Na ukiona kijana mwenye nguvu anatamka kuwa hayo majumba ni
ya mafisadi, fahamu kuwa familia yake na jamii inayomzunguka iko msibani. Si
tetei wizi ama ufisadi na si sahihi kuwa mwizi au fisadi. Na ni dhambi hata kwa
mungu wezi waadhibiwe tena vikali.
Lakini, pia sikubaliani na mtazamo kwamba kila anayefanikiwa
ni mwizi au fisadi. Kuna watanzania wengi tu ambao wanakesha, wanafikiri na
kubuni mbinu za kufanikiwa huku wakiongozwa na jitihada kubwa ya kufanya kazi
na kuchangamkia fursa ndani na nje ya nchi na kutumia pesa kwa kwa makini katka
uwekezaji binafsi bila ufujaji.
Hawatapanyi mapato kwa starehe na kuulimbukia utandawazi.
Kila senti yao
inatumika kwa tija na manufaa. Hawa wanastahili pongezi siyo kuitwa wezi. Kazi
kubwa tliyonayo hasa vijana ni kutambua vipaji vyetu na kuvitumia
ipasavyo.Tpunguze kulalamika tuongoze juhudi zetu katika ufanya kazi zaidi.
Tutafanikiwa sana
maishani.