Leo tunaye msanii wa filamu za Kibongo, Wema Sepetu ambaye
hivi karibuni alithubutu kugombea ubunge kupitia viti maalum mkoani Singida.
Kwa bahati mbaya kura za msanii huyu hazikutosha. Mwandishi
wetu alionana na mwanadada huyo nyumbani kwake Kijitonyama jijini Dar na
kumpiga maswali 10 mujarabu. Ungana nami…
Ijumaa: Hongera kwa kujitosa kwenye siasa, nini kilikusukuma
kuingia huko?
Wema: Nilikuwa nashauku ya kuwa mheshimiwa, hata baba yangu
aliwahi kuniambia naweza hivyo nikajaribu bahati yangu.
wema (8)Ijumaa:
Ukiacha marehemu baba yako, nani alikupa sapoti kubwa na ukajiona unaweza?
Wema: Namshukuru mama yangu, alinipa sapoti kubwa nikajiona
naweza kwani alinitoa hofu niliyokuwa nayo.
Ijumaa: Unadhani kipi kimekuangusha kwenye uchaguzi ule?
Wema: Uchanga wangu kwenye siasa lakini naamini muda ulikuwa
bado.
Ijumaa: Ingawa hukufanikiwa kupata nafasi ya ubunge
umejifunza nini kupitia siasa?
Wema: Kwa kweli nimejifunza vitu vingi maana haviendani hata
na umri wangu na nimepata ujasiri mkubwa. Kikubwa ukiingia kwenye siasa
ujipange sana .
Ijumaa: Je, kwa hatua uliyoifikia unategemea kuendelea na
siasa?
Wema: Niache? Siwezi kwani itakuwa kazi yangu, kama gari ndiyo limewaka sasa.
Ijumaa: Najua siasa ni hela hasa kipindi cha kampeni,
uliwezaje kumudu gharama zote?
Wema: Ni rahisi sana
ukiwa na watu wanaokupenda, walijitokeza watu kunichangia kwa ajili ya
kuhakikisha nafanikiwa. Siwezi kuwataja lakini nawashukuru sana .
Ijumaa: Tulipata habari kwamba baada ya kushindwa uliangua
kilio, kwa nini?
Wema: Unajua unapoenda kufanya kitu lazima una matumaini
japo kuna kushindwa lakini kushinda ndiyo lengo sasa usipofanikisha lazima roho
inauma.
Ijumaa: Ulijisikiaje ulipokuta nyomi la watu wakikusubiri
kwa ajili ya kukupokea wakati hukuwa umeshinda?
Wema: Niliamini nina watu wengi ambao wananipenda na
nilijifunza mengi kupitia ujio wao, pia walinitia moyo wa kuendelea na siasa.
Ijumaa: Kuna madai kuwa baada ya kushindwa una mpango wa
kuhamia Ukawa, hilo
unalizungumziaje?
Wema: Ninachojua watu wa Ukawa wamenitafuta na ilikuwa
tukutane jana (Jumatatu) ila tutakutana Jumatano (juzi), nikijua wanachoniitia
ndiyo nitafanya uamuzi.
Ijumaa: Baada ya kuingia kwenye mambo ya siasa tumtegemee
Wema wa aina gani?
Wema: Mtarajieni Wema wa tofauti na yule mliyemzoea, mambo
ya skendoskendo hayatakuwa na nafasi kwenye maisha yangu.