Staa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ akiwa
na mashabiki wake.
Waandishi Wetu
Kufuatia kupigwa mwereka kwenye Ubunge wa Viti Maalum
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Singida, staa wa sinema za Kibongo,
Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ amekiri kwamba kilichomponza katika kinyang’anyiro
hicho ni skendo za ngono hivyo kwa sasa atakuwa makini ili asichafuke.
MAPOKEZI
Akizungumza na gazeti hili baada ya kupokelewa kishujaa na
kuacha historia jijini Dar aliporejea kutoka Singida wikiendi iliyopita, Wema
alisema mashabiki wake hawatamsikia tena na skendo hizo huku akiahidi kuibuka
na bonge la ‘surprise’
UMAKINI
“Shukurani zangu zipo palepale kwa mashabiki wote
wanaonisapoti.
“Ninachowaahidi kwa sasa ni kuwa makini na skendo lakini pia
kuna kitu cha kushtua nitafanya hivi karibuni ambacho kitaibua surprise
(mshtuko) nzito kwa mashabiki wangu,” alisema Wema.
TEAM WEMA
Katika mapokezi hayo ambayo gazeti hili lilikuwa mstari wa
mbele, makundi ya mashabiki wake na yale ya Team Wema yalipeana taarifa kupitia
mitandao ya kijamii kuwa kipenzi chao, Wema angefika Dar, Jumapili iliyopita
ambapo taarifa zilisema kuwa walikutana kimyakimya na kuandaa mapokezi ya
Madam.
Mishale ya saa 7:00 mchana ndipo Team Wema na mashabiki wake
wengine walianza kumiminika maeneo ya Kimara-Baruti jijini Dar wakiwa na mabasi
ya kukodisha, pikipiki na magari binafsi ambapo shamrashamra za kila aina
zilifanyika.
KIBAO-KATA
Pia kulikuwa na ngoma ya Kibao-Kata, michezo ya pikipiki
huku nyimbo za kumsifu Wema zikiimbwa.
SHANGWE
Umati uliojitokeza walianza kulipuka kwa shangwe baada ya
kumuona Meneja wa Wema, Martin Kadinda aliyeingia katika eneo hilo akifuatiwa na Petit Man ambaye
alifuatana na wasanii wa Bongo Fleva, Mirror na Suma Mnazareti.
MJAMZITO
Mashabiki hao wa kila kada huku watoto wakifurika kumuona
Wema walionekana kuwa na mapenzi ya hali ya juu huku mama mmoja mwenye ujauzito
mkubwa akionekana akijichanganya kila kona bila kujali hali yake.
WEMA ENEO LA TUKIO
Wema aliingia katika maeneo hayo (Kimara-Baruti) akiwa ndani
ya gari aina ya Toyota Land Cruiser ambapo alishuka na kuingia ndani ya BMW
lililoletwa kumpokea ambapo alitokea kwenye paa na kuanza kusalimia mashabiki
wake waliolipuka kwa furaha na wengine wakiangua kilio cha furaha.
MABUSU
Kuna wengine walishindwa kujizuia wakajikuta wakimfuata Wema
wakimbusu na kumshika nywele zake kama vile
siyo binadamu.
CHENI NA PETE
Wema alilazimika kugawa cheni na pete zake za dhahabu kwa
mashabiki wake ili kuwatuliza huku akiwashukuru kwa kumpokea na kuwaaga kuwa
anakwenda nyumbani kwake Kijitonyama ambapo msafara wake ulisababisha foleni ya
zaidi ya robo saa njia nzima ambapo alikuwa akisindikizwa na pikipiki.
“Yaani Madam amepokelewa na watu kama
rais vile, duh! Sijawahi kuona, amekosa ubunge lakini shamrashamra yake kama vile ameshinda!” Alisema mmoja wa mashabiki wa Wema
aliyevalia fulana zenye nembo iliyoandikwa ‘Wema’.
KINACHOONEKANA
Habari zilieleza kwamba, kinachoonekana Wema anajipanga upya
ili kujiimarisha kisiasa kwa ajili ya baadaye hivyo atajitahidi kuwa mbali na
skendo hasa za wanaume.
TUJIKUMBUSHE
Huko nyuma Wema aliwahi kuripotiwa kubadili wanaume
mbalimbali wakiwemo; Jumbe Yusuf Jumbe, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Charles Gabriel
‘Chaz Baba’ na CK.