Aliyekuwa mgombea Urais wa CCM ambaye pia ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya chama hicho, Januari Makamba, jana alimshukia mgombea urais
kwa tiketi ya Ukawa, Edward Lowassa kwamba ni mroho wa madaraka.
Makamba alitoa kauli hiyo katika viwanja vya Barafu mjini Dodoma wakati akimnadi
mgombea ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde. January alisema kuwa
Lowassa ameivuruga demokrasia ndani ya Chadema na kupeleka mizengwe itakayokiua
chama hicho na umoja wao.
“Yale siyo mabadiliko kama
wanavyojinadi bali ni uroho wa madaraka kwa mtu mwenye uroho na chama chenye
uroho, lakini hawezi na hawawezi kushika madaraka ya kuongoza nchi,” alisema
Makamba.
Alisema kinachoendelea kwa vyama vinavyounda Ukawa ni
maigizo na siyo mabadiliko ya kweli kwa sababu mgombea urais ametoka CCM na
Sera za CCM na mgombea mwenza ametoka CUF na sera za huko, hivyo hawawezi
kuungana kwa pamoja kwa sababu hawajui nini maana ya kile wanachogombea.
Hata hivyo, Makamba alikiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni
mgumu kuliko uchaguzi wowote uliowahi kutokea katika mfumo wa vyama vingi na
akawataka wana CCM kujiandaa kikamilifu.
Alisema CCM kinapaswa kuwa makini na imara wakati wote ili
kutoyumba na wakifanya hivyo watajikuta wanapata mchanganyiko ambao utaleta
shida katika maendeleo.
Kwa upande wake mgombea ubunge Mavunde alijipachika jina la
Mr Makao akisema lazima ataipelekea Dodoma hadhi
ya kweli katika kufikia makao ambayo yamekuwa yakisemwa kama
hisani.
Mavunde aliomba wananchi kumwamini na kumpa nafasi hiyo
kwani ana uhakika kwa miaka mitano ataifanya Dodoma kupaa kiuchumi huku akisema
atashughulika na watu wenye kipato cha chini pamoja na kumaliza migogoro ya
ardhi.