Maoni: Vyombo Vyetu Vya Habari Viikumbuke Historia Ya Rwanda

Tarehe 7, April ya mwaka 1994 ni mwaka wenye kumbukumbu ya simanzi na yenye kutia uchungu katika historia ya mwanadamu hapa duniani, kwani ni mwaka ambao watu takribani 800,000 waliuawa ndani ya siku mia moja.

Ni katika nchi ya Rwanda ambayo ilishuhudia raia wake, wanawake, kwa watoto wakiuuawa katika hali isiomithilika kutokana na uroho wa madaraka waliokuwa nao watawala wake.

Pamoja na kuelezwa kuwepo kwa chuki za kikoo baina ya Wahutu na Watusi, haki za watu kukandamizwa kama  vyanzo vikuu vya mauaji hayo yalioitwa ya kimbari (Genocide), pia vyombo vya habari vimewekwa katika kumbukumbu za kihistoria kuwa miongoni mwa vyanzo  vikuu vya mauaji na mateso ya raia wa Rwanda wasiokuwa na hatia.

Katika mauaji hayo ya kimbari vyombo vya habari ambavyo vingine wahusika wake walifikishwa mbele ya mahakama maalumu ya Arusha na kukutwa na hatia, vilitangaza na kuchapisha habari zilizojaa chuki dhidi ya wanyarawanda wenyewe, mfano wa gazeti la Kangura, Radio RTLM ambavyo viliandika kuwa watusi ni mende na walitakiwa kuangamizwa.

Na jambo la kusikitisha sana mataifa na wale wanaojiita kuwa ni  watetezi wa haki za binadamu hawakufanya jitihada zozote ili kuokoa roho hizo zilizoangamizwa, bali walikaa pembeni wakiangalia ushenzi na unyama ukifanywa na watu waliokuwa na roho za kishetani.

Katika kauli ya ukakasi, Rais wa wakati huo wa Marekani, Bill Clinton alisema kuwa hawangeweza kuingilia kati kuvizuia  vyombo vya  habari vilivyokuwa vikichochea mauaji kwa hoja kuwa vilikuwa vinatumia haki zao za uhuru wa habari.

Hiyo ni miaka 21 iliopita, iliowaacha wanyarwanda na makovu ndani ya mioyo yao ya kuwapoteza ndugu, jamaa, wazazi na mali zao huku wengine wakifanywa wakimbizi nje ya nchi yao walioipigania toka mikononi mwa wakoloni wa Ubelgiji.

Vyombo vyetu
Wakati wenzetu wakiwa tayari na historia hiyo mbaya, yenye kutia uchungu, hapa kwetu vyombo vyetu vingi vya habari vinaonekana kuisahau kabisa historia  hiyo.
Ukiwa huu ni mwaka wa uchaguzi uliojawa na hamasa ya aina yake kutoka kwa wananchi, vyombo vyetu vingi vya habari hapa nchini navyo vimejikuta vikikumbwa na ushabiki wakisiasa walionao wananchi wengi kwa sasa.

Vyombo vyetu vingi vya habari kwa sasa vinaonekana kuitupilia mbali  misingi na maadili yao ya kazi, ikiwemo ya uwazi, uadilifu na kutokuwa na upendeleo (Objectivity), ushabiki kipindi vinapoandika habari zao nyingi zikiwemo za kisiasa.


Vimejisahau kuwa navyo ni sehemu ya jamii na vinapaswa kuitumikia jamii kwa kuhakikiksha vinaandika habari zenye kuilea na kuijenga jamii katika msingi ilio bora isiokuwa na mitafaruku inayozalishwa na vyombo hivyo.

Ninasema vimejisahau, kwani tayari tumeanza kuziona habari zenye viashiria vya chuki kwa jamii, mfano ni ile habari ilioandikwa na moja ya magazeti ya muda mrefu hapa nchini eti kuwa wananchi waliojitokeza kwenda kumsindikiza mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Ndugu Edward Lowassa kwenda kuchukua fomu  eti walikuwa ni vibaka, kichwa cha habari kikasomeka, “Vibaka watikisa jiji la Dar Es Salaam”.
Gazeti lingine mara baada ya CCM kutangaza timu ya watu wake wa kampeni, likaandika habari yenye kichwa cha habari kuwa  “CCM Yaunda timu ya ‘kumtusi’ Lowassa.”

Zipo habari nyingi tu zimekuwa zikiandikwa kwa mrengo ambao ni wa kiushabiki na usio na ukweli wowote, kama kweli wale wafuasi wa Lowassa ingethibitika ni vibaka kweli, hakuna jinsi ukweli lazima usemwe, na kama kweli timu ya CCM  ni ya kumtusi Lowassa, hakuna jinsi lazima ukweli usemwe.

Ila sidhani kama kuna chombo hata kimoja kati hivyo, kina ushahidi wa habari zao hizo, kama sio ushabiki tu usio na maana, kama ni uchambuzi nadhani nafasi yake ilikuwa ni kwenye makala japo nako huko ukweli huzingatiwa pia sio uchambuzi tu.

Na kama inavyofahamika, miongoni mwa nadharia zinazozungumzia jinsi vyombo vya habari vinavyoathiri hadhira zao  ni ile iitwayo nadharia ya risasi (Magic Bullet Theory) ambayo athari(ujumbe) zake huwafika walengwa kama risasi na kwa kuamini moja kwa moja kile kilichoandikwa pasi na kuifanyia tathmini ya kina habari hiyo.

Na kama nilivyotanabaisha hapo juu kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, ambao umejawa na hamasa na ushabiki wa aina yake, hivyo wananchi wengi wamebaki kuwa ni wakupokea na kuamini kila kinachosemwa, hawataki kufanya tafakari dhidi ya habari husika, ilimradi iko upande wake.

Mfano, mara baada ya kuandikwa kwa habari hiyo ya kuwa timu ya kampeni ya CCM ni ya kumtusi Lowassa, nilikuwa katika sehemu wanapouza magazeti hapa jjini Dar Es Salaamu, nilichokiona wengi waliiamini habari hiyo na ubishi mkubwa ukazuka baina ya wafuasi wa vyama huku kauli ikiwa “Wajaribu kumtusi Lowassa waone.”

Uhariri hatari
Pia nimeshangazwa sana kumuona mmoja wa wahariri hapa nchini wakati akiongea kwenye runinga moja hapa nchini , akitetea vyombo vya habari vya kibinafsi kuchukua upande  kwa kuandika habari kama wao wanavyotaka, huku akitilia mkazo tu kwa vyombo vya habari vya umma ndio vinapaswa kuandika habari zenye usawa bila kupendelea chama chochote.

Nadhani alijasahau kwani kwa mujibu wa misingi na maadili ya uandishi wa habari, ni wajibu wa kila mwandishi wa habari na chombo cha habari bila kujali hiki ni cha kibinafsi, na kile ni cha umma kuandika habari yeneye ukweli, mizani sawa na kutokuwa na upendeleo (impartiality).

Bado kuna muda
Hadi hapa tayari vyombo vya habari vimeshaanza kuigawa jamii kulingana na habari vinavyoandika, na huu ni mwanzo tu, kampeni ndio zimeanza. Bila kuwakumbusha wahusika wa habari tutegemee habari nyingi za kuigawa jamii.

Mwisho wake unaweza kuwa ni mbaya,  hivyo vyombo vyetu navyo vikumbushwe historia hii ya Rwanda. Visije vikatupeleka huko.