MWENYEKITI wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji
Christopher Mtikila, amesema chama chake kinaandaa taratibu za kwenda
mahakamani ili kumshtaki mgombea urais mteule wa CCM, Dkt.
John Magufuli na mgombea urais wa CHADEMA, Bw. Edward Lowassa.
Alisema wagombea hao kwa nyakati tofauti, wameshiriki
kuiingizia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha ambapo wanasheria wa chama
hicho wapo katika hatua za mwisho ili wafunguliwe mashtaka mahakamani.
Mchungaji Mtikila aliyasema hayo Dar es Salaam jana, alipozungumza na
waandishi wa habari akisisitiza kuwa, wagombea hao wamepoteza sifa za kuwania
nafasi hiyo akidai hawana vigezo kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kuwa, Bw. Lowassa, anahusishwa na sakata la
kampuni ya kufua umeme ya Richmond na kuishangaa
CHADEMA akidai chama hicho kilipata umaarufu wa kupinga vitendo vya ufisadi
lakini wamempokea Bw. Lowassa na ana tuhuma kama
hiyo.
"Kipindi cha nyuma, CHADEMA walianzisha operesheni
nyingi ikiwemo ya Sangara na Movement for Change zikiwa na lengo la kupinga
ufisadi, kwanini wamempokea Lowassa waliyemuita fisadi.
"Hii ina maana
kuwa, ndani ya CHADEMA hakuna siasa, nawapongeza baadhi ya viongozi wa chama
hicho na wanachama wao ambao kimsingi hawakubaliani na matakwa ya viongozi wa
juu,"
Akimzungumzia Dkt. Magufuli, alimhusisha na tuhuma ya
uuzwaji wa nyumba za Serikali akidai kitendo hicho kimeisababishia hasara
Serikali lakini hakupelekwa mahakamani kwa kutumia madaraka yake vibaya kama ilivyokuwa kwa Basil Mramba, Daniel Yona ambao hivi
sasa wanatumikia kifungo gerezani.
Alisema nyumba hizo zilikuwa makazi ya viongozi kama Majaji, Makatibu Wakuu na Watendaji waandamizi
serikalini ambao wengi wao walilazimika kuishi hotelini kwa gharama za Serikali.
