Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete
amesema baadhi ya kauli zinazotolewa na Umoja wa Vyama vya Upinzani (Ukawa),
zinaashiria uvunjifu wa amani pindi matokeo ya kura yatakapoanishwa baada ya
zoezi la upigaji kura Oktoba 25 mwaka huu.
Rais Kikwete alisema baadhi ya kauli hizo zimekuwa
zikionyesha wazi viashiria vya uvunjifu wa amani na upotoshaji kwa kundi kubwa
la vijana ambao wanapiga kura kwa mara ya kwanza.
Akizungumza wakati akizindua Kampeni ya Mama Ongea na Mwanao
jijini Dar es Salaam Rais Kikwete alisema;
“Wamediriki kusema
wazi bila kificho kwamba patakuwa hapatoshi, hizi ni kauli zinazoashiria
uvunjifu wa amani. Tunachokisema CCM ushindi kwetu ni lazima na tutashinda kwa
kishindo na kwenda nginja nginja mpaka Ikulu.”
Kikwete alisema CCM imejipanga kuhakikisha inapata ushindi
katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuongeza kuwa ili kufanikisha hilo wamepanga kikosi kazi ambacho kitatembea
nyumba kwa nyumba, chumba kwa chumba, mtu kwa mtu ikiwa kwa sasa tayari
wameshaanza kufanya kampeni zao kupitia mtandao ya simu za mkononi.
Katika hafla hiyo ya kuzindua kampeni hiyo inayoratibiwa na
msanii wa filamu na Miss Tanzania
mwaka 2006, Wema Sepetu, Rais Kikwete aliwataka wanawake kaungalia mazuri yote
yaliyofanywa na Serikali ya CCM katika kumuinua mwanamke.