Mara nyingi huwa inakadiriwa kuwa biashara nyingi mpya
zinazoanzishwa, huwa zinajikuta zinakufa
kabla hazijafikia miaka mitano na chache huwa ndio zinazoendelea baada ya hapo.
Kufa huku kwa biashara hizi huwa hakuji kwa bahati mbaya, bali huwa kunatokana
na sababu kadhaa ambazo pengine huwa zinatokana na wajasiriamali wenyewe au nje
ya wajasiriamali. Ni muhimu kujua sababu zinazopelekea biashara nyingi zife
kabla hazijafikisha miaka mitano, ili kama upo
kwenye mchakato wa kuanzisha biashara ama upo kwenye biashara usije ukafanya
makosa hayo na kujikuta umeua biashara yako.
Hizi Ndizo Sababu 10
Zinazofanya Biashara Nyingi Mpya Zishindwe Kuendelea.
1. Usimamizi mbovu.
Hili ndilo kosa kubwa huwa linafanyika kwa biashara nyingi
na matokeo yake ni kuwa ni biashara za kawaida ambazo hazina mafanikio makubwa sana na mwisho wa siku
kufa kabisa. Kunapokosekana usimamizi mzuri na wa kutosha, mara nyingi biashara
huanza kujiendea kiholela ama kwa mazoea ya kawaida tu, kitu ambacho ni hatari sana kwa biashara. Ni
muhimu kwa biashara ikawa na usimamizi mzuri na mipango iliyotulia ili iweze
kuleta faida na mafanikio makubwa, vinginevyo itakufa.
2. Kukosekana kwa
ung’ang’anizi.
Mara nyingi huwa inachukua muda mrefu kidogo kwa biashara
mpya, kuweza kukuletea faida kama ulivyokuwa
umepanga. Katika kipindi hiki huwa ni kipindi kigumu kwa wajasiriamali wengi,
kwani ni kipindi ambacho biashara huwa inajiendesha kwa faida kidogo sana na uvumilivu wa hali
ya juu huwa unahitajika. Hapa ndipo, biashara nyingi mpya huwa zinakufa ama
kushindwa kuleta mafanikio makubwa, kutokana na kukosekana kwa ung’ang’anizi
ambacho huwa ni kitu muhimu sana .
3. Kuweka
biashara katika eneo lisilo sahihi.
Hii ni moja ya sababu muhimu sana ambayo mara nyingi huwa inapelekea
biashara nyingi mpya kufa. Unapoweka biashara yako katika eneo lisilo sahihi,
mara nyingi kitakachotokea utaanza kukosa wateja na utajikuta unabaki kulaumu
kuwa biashara hiyo hailipi au haifai kumbe eneo uliloweka ndilo sio sahihi. Ili
kuepuka hili, ni muhimu sana
kuiweka biashara yako katika eneo lililosahihi ambapo una uhakika unaweza
kupata wateja, ambao watasaidia kuifanya biashara yako kuwa hai.
4. Biashara inakuwa
haitatui matatizo mengi ya watu.
Lengo kuu la biashara sio kupata faida pekee, bali ni pamoja
na kutatua matatizo ya watu. Kwa jinsi biashara inavyozidi kutatua matatizo
mengi ya watu ndivyo inavyozidi kupata wateja wengi na faida kuwa kubwa zaidi.
Hakuna biashara yoyote duniani ambayo imeendelea bila kutatua matatizo muhimu
ya watu. Kama unataka kufanikiwa na kupiga
hatua kwa biashara unayofanya, ni lazima
biashara yako itatue matatizo ya watu kwa sehemu kubwa.
5. Kushindwa
kujifunza kutokana na makosa.
Ni ukweli usifiochika wajasiriamali walio wengi huwa ni watu
wa kufanya makosa katika biashara zao. Lakini, pamoja na makosa hayo kitu pekee
ambacho huwa kinawafanya wananyanyuka na kusonga mbele ni kile kitendo cha
kuchukua hatua ya kujifunza na kujirekebisha kutokana na makosa hayo. Tatizo
walilionalo wajasiriamali wapya, huwa ni wazito kujifunza kutokana na makosa na
kujikuta ni watu wa kurudia makosa yale yale yanayopelekea kuua biashara zao.
6.Kukabiliwa na
ushindani mkubwa.
Biashara nyingi mpya huwa zinashindwa kufanya vizuri sokoni
kutokana na kukutana na ushindani wa hali ya juu. Kunapokuwa kuna ushindani wa
kisoko, halafu wewe ukiwa kama mjasiriamali ukashindwa kusoma nyakati za jinsi
gani unaweza kukabiliana hali hiyo, uwe na uhakika biashara yako haiwezi
kufanikiwa sana ,
zaidi baada ya muda itaanza kupotea polepole na mwisho ni kufa kabisa.
7. Kutokuwa na mtaji
wa kutosha.
Kutokuwa na mtaji wa kutosha katika biashara, hii pia huwa
ni sababu mojawapo inayopelekea biashara nyingi mpya kufa mapema. Mtaji huwa
unahusika sana
hasa pale unapohitaji kuongeza pengine bidhaa ili kuweza kukabiliana na soko na
wakati huohuo unakuwa hauna pesa ya kutosha. Inapotekea hali hii ya kukosa
mtaji wa kutosha kwa biashara unayoifanya, hapo ndipo huwa mwanzo wa kushindwa
kwenye ushindani na biashara huanzia kuyumbia hapo na baadae kupelekea kufa, kama jitahidi nyingine za ziada zisipofanyika.
8. Kunafanya biashara
na watu ambao sio sahihi.
9. Mipangilio mibaya
ya bei.
Mara nyingi biashara nyingi zinazoanza huwa zinamipangilio
sio mizuri ya bei kitu ambacho husababisha kuwachanganya wateja. Hili huwa
linatokea pengine kutokana na kupanga bei ya bidhaa, pasipo kujali ama
kuangalia ubora wa bidhaa husika, hali ambayo husababisha wateja kuingiwa na
shaka na kuanza kuhama kidogo kidogo, kitu ambacho ni hatari sana kwa biashara kuweza kuendelea.
10. Kukosa ushauri
mzuri wa Kibiashara.
Mjasiriamali unapokosa ushauri mzuri ambao
ungewezakukusaidia kuifanya biashara yako ikawa hai, kinachotokea hapo ni kuua
biashara. Biashara nyingi huwa zinakufa kwa sababu ya kupokea ushauri wa kila
aina na kuufanyia kazi hata kwa watu ambao sio wazoefu sana wa biashara husika. Kama
unataka biashara yako iweze kusonga mbele na kuleta matunda acha kupokea
ushauri wa kila aina, vinginevyo utaua biashara yako.
Mwisho, zipo sababu nyingi zinazopolekea biashara nyingi
mpya kutoweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa na kupelekea nyingi kuweza kufa
hata kabla ya kufikisha miaka mitano. Kwa kuanzia, hizo ndizo baadhi ya sababu
zinazofanya biashara nyingi kuweza kufa na kushindwa kusonga mbele kabisa. Ni
muhimu kuweza kujifunza na kuchukua hatua zitakazotusaidia kuepuka makosa hayo
na kuweza kufanikiwa.