Tunaishi kwenye dunia ambayo ina kelele nyingi sana . Katika kipindi hiki
ambacho tunaishi, kwa siku moja unakutana na taarifa nyingi kuliko taarifa
ambazo mtu aliyeishi miaka ya 1800 alikuwa anakutana nazo mwaka mzima, na
wakati mwingine kwa kipindi chote cha maisha yake.
Tunaishi kwenye kipindi cha mapinduzi ya taarifa, kwa hivyo
tungetegemea taarifa hizi ziwe msaada mkubwa kwetu kupiga hatua kwenye jambo
lolote ambalo tunafanya, iwe ni kazi, biashara au hata maisha ya kawaida tu.
Lakini hali halisi sio, taarifa hizi nyingi zimekuwa kikwazo
cha sisi kuweza kupiga hatua. Na ni kwa sababu hatujachukua muda wa kuchambua
ni taarifa zipi muhimu kwetu na zipi sio muhimu.
Taarifa tunazokutana nazo ni nyingi sana ,
na nyingi zinashika hisia zetu, zinakazana kupata muda wetu, vichwa vyenyewe
vya taarifa hizi vinavutia sana
na hatimaye unajikuta ukisoma au kusikiliza taarifa hiyo. Unamaliza kufuatilia
taarifa hiyo, hakuna cha ziada ulichoongeza na umepoteza muda wako.
Taarifa ambazo zilipaswa kuwa ukombozi kwetu, zimegeuka na
kuwa sumu kwetu, na tatizo sio taarifa hizi, bali matatizo yanaanzia kwetu sisi
wenyewe.
Mtu unaamka asubuhi na cha kwanza unachofanya ni nini,
unakamata simu na kuanza kuperuzi mitandao, unapata habari mbili tatu za
kukusisimua. Unatoka kuelekea eneo lako la kazi, njiani unaendelea kupata
taarifa, unafika eneo la kazi na kabla hujaanza kazi unaangalia tena ni nini
kinaendelea. Ufuatiliaji huu mzuri wa habari mbalimbali ungekuwa mzuri sana kama zingekuwa ni
habari ambazo zinakuongezea maarifa na kukufanya uongeze thamani zaidi, lakini
sivyo.
Unafuatilia habari nyingi huku uzalishaji wako kwenye kazi
unayofanya ukiwa mdogo sana
na hivyo kushindwa kutoa thamani ambayo itakufanya ulipwe zaidi. Unaweza
kulalamika sana
lakini taarifa hizi unazokazana kufuatilia ndio adui yako namba moja wa wewe
kushindwa kuwa na ufanisi mzuri kwenye kazi.
Ufanye nini sasa?
Je umechoshwa na hali hii ya kuwa mtumwa wa taarifa? Je
unaona kama huwezi kujizuia kuangalia simu
yako kila baada ya dakika chache? Kama ndio karibu sana
hapa utajifunza njia ambazo kama utazitumia utaweza kuondokana na tatizo hilo . Kama
bado hujawa tayari kubadilika, na unaona unachofanya kipo sawa kwako unaweza
kuishia hapa kwa sababu ukiendelea mbele utanichukia bure, kwa sababu
nitakueleza ukweli ambao hutaki kuusikia. Ndio najua hutaki kuusikia kwa sababu
kwa wakati fulani nilikuwa hapo ulipo wewe na nilikuwa nafikiri unavyofikiri
wewe, lakini nilipohitaji kweli mabadiliko nilichukua hatua.
SOMA; Changamoto Mbili Kubwa Utakazokutana Nazo Wakati Wa
Mabadiliko.
Leo nitakupa tabia unazohitaji kujijengea ili kuongeza
uzalishaji wako katika ulimwengu huu uliojaa kelele nyingi za taarifa. Soma kwa
makini nimesema tabia kwa sababu mara nyingi watu tunapenda MBINU, lakini
nimejifunza kwamba mbinu huwa hazidumu, mbinu ni za muda mfupi. Sasa tukipeana
mbinu hapa ambazo ni za muda mfupi, changamoto hii ya taarifa haiishi leo wala
kesho, kwanza kadiri siku zinavyokwenda ndivyo taarifa zinavyoongezeka. Hivyo
mbinu hazitakusaidia, unahitaji kujenga tabia.
Mbinu ni rahisi kujenga, lakini ni vigumu kudumu nazo. Tabia
ni ngumu kujenga lakini ni rahisi kuishi nazo.
1. Kuwa na orodha ya
vitu utakavyofanya kwa siku husika.
Usianze siku yako kama mwendawazimu, kama
unaanza siku yako bila ya kuipanga, umeamua kuipoteza siku yako. Kabla ya
kulala, andika ni mambo gani utakwenda kufanya siku inayofuata, au unapoamka
asubuhi na mapema, panga ni mambo gani unakwenda kufanya siku hiyo.
Kuwa na orodha ya vitu ambavyo utafanya, tena orodha
iliyoandikwa, itakufanya uwe makini zaidi katika kutekeleza yale
uliyoorodhesha. Na ili kuhakikisha unafuatilia orodha hiyo kwa umakini, mwisho
wa siku weka alama ya vema kwa yale uliyofanikiwa kuyafanya na alama ya mkasi
kwa yale ambayo hukufanya. Ukifanya hivi kila siku utajikuta unalazimika
kufuata orodha yako.
Na orodha hii iandikwe kwenye kitabu chako cha kumbukumbu
(notebook au diary).
Narudia tena kama unaianza siku yako unaipangilia hutakuwa
na tofauti na mwendawazimu, kwa sababu kama
huna cha muhimu cha kufanya utajikuta unapokea chochote ambacho dunia
inakurushia kupitia habari nyingi zinazoendelea.
Unashangaa unaamka asubuhi na mapema, siku ya kazi badala ya
kushambulia majukumu yako unaanza kushambulia watu kwenye mitandao, huyu
kafanya hiki, huyu kakosea kile na mengine mengi ambayo sio muhimu kwako.
2. Usianze siku yako
kwa habari.
Ndio, namaanisha hivi asubuhi na mapema usianze siku ya ko
kwa kusikiliza au kusoma habari. Kama
unapingana na hili acha tu kusoma na nenda kasome habari.
Siku moja nikiwa nafundisha semina niliwaambia watu hili na
mtu akanipinga na kusema utawezaje kuanza siku bila ya kujua ni kitu gani
kinaendelea. Nikamwambia sawa, umeamka asubuhi na kukimbilia gazeti na habari
kubwa ni kwamba kuna mtu kamnyonga mke wake na yeye mwenyewe kajiua, sasa
habari kama hii inakusaidia nini kwenye siku
yako ya kazi? Sana sana
inakufanya uianze siku yako ukiwa unajisikia vibaya na kama
utaanza siku hivi huwezi kuwa na uzalishaji mzuri.
Kwa hiyo tunakubaliana kwa hili, hakuna habari asubuhi. Kama
unaweza kufanya hivyo siku nzima vizuri sana , kama huwezi pitia habari baada ya kazi zako za msingi.
Tumia muda mwingi kujifunza vitu ambavyo vitakuongezea
maarifa na sio vitakavyokusisimua na kukuacha ukiwa unajisikia vibaya.
3. Kaa mbali na simu
wakati wa kazi muhimu.
Lakini nitakosa dili kama
sitakuwa na simu karibu. Hiko ni kitu kingine ambacho unajidanganya nacho na
hivyo kujikuta unasumbuliwa kila mara kwa kuwa na simu yako karibu. Kama unafanya kazi ambayo inahitaji utulivu, ni vyema
ukakaa mbali na simu yako, au izime au iweke kimya kabisa. Hii itakupa nafasi
nzuri ya kuweka akili yako yote kwenye kazi unayofanya na sio kufikiria meseji
iliyoingia nani atakuwa ameituma.
Na uzuri ni muda mfupi tu ambao utahitaji kufanya hivi na
ukaongeza ufanisi mkubwa kwenye kazi zako.
Jibu kwa wale ambao wanafikiri kukaa mbali na simu
watapoteza dili, sio kweli, hakuna dili utakayopoteza kwa kuwa mbali na simu
yako kwa muda mfupi. Kama kuna mtu anakuhitaji
kweli atakutafuta tu na pia atakupata.
Kwa mfano mimi sehemu kubwa ya kazi zangu nafanya kwa njia
ya simu, hivyo nilikuwa nafikiri inabidi niwe na simu masaa 24. Nilipoanza
kutenga muda wa kuwa mbali na simu, nilikuwa nakuta simu nyingi zimepigwa, kila
nilipokuwa najaribu kuwapigia watu wale walionikosa, wengi wanakuwa wamesahau
hata walikuwa wanataka nini.
Kuna siku mtu alikuwa ananitafuta kwa ajili ya kwenda
kufundisha semina, nilikuwa mbali na simu na niliposhika simu nilikuta amepiga
simu kama mara tano na akatuma ujumbe, tafadhali nitafute nina jambo la muhimu sana . Na likawa muhimu
kweli.
Nataka nikutoe wasiwasi kwamba kuwa mbali na siku
hakutakukosesha wewe dili, bali kutakufanya upate dili bora zaidi na wakati huo
ukiwa na uzalishaji na ufanisi mkubwa.
Kuwa na orodha, usianze siku kwa habari, kaa mbali na simu,
ni vitu vigumu kwako? Tumalizie na kingine muhimu.
4. Fanya kazi kwa
vipaumbele na anza na majukumu makubwa na magumu.
Umewahi kujikuta siku inaisha halafu hujui umefanya nini?
Unajiona ulikuwa bize lakini mwisho wa siku huoni kitu kikubwa ambacho
umekifanya? Basi hiyo inatokana na kukosa vipaumbele kwenye kazi zako.
Usikimbilie kufanya majukumu ambayo ni rahisi, mara nyingi
haya yanakuwa na thamani ndogo, halafu yatachukua muda wako ambao ndio unakuwa
na uzalishaji mzuri. Anza na yale majukumu makubwa asubuhi na ukiyamaliza
utakuwa umeongeza uzalishaji wako na ufanisi pia.
Kumbuka hizi tumejadili hapa sio mbinu, bali ni tabia. Ni
tabia kwa maana kwamba unahitaji kuzifanya kila siku. Inabidi ifike mahali iwe
ni sehemu ya maisha yako kwamba ni lazima upange siku yako kabla hata
hujaianza, usianze siku kwa habari, kuwa mbali na simu unapohitaji utulivu na pia
kufanya mambo muhimu kwanza.
Mambo haya yanapokuwa tabia kwako utakuwa na uzalishaji
mkubwa na ufanisi mzuri, halafu utakuwa na mafanikio makubwa sana kwenye kazi au biashara unayofanya.
Kama mambo haya ni magumu kwako kufanya unaruhusiwa
kuendelea kufanya kile ambacho umezoea kufanya, lakini wakati unafanya hivyo
tafadhali sana
usituletee kelele kwamba maisha magumu, kipato kidogo na kelele nyingine nyingi
ulizozoea kupiga. Una haki ya kuchagua maisha ambayo ni bora kwako kuishi,
usikubali kuendelea na maisha ya kuburuzwa, panga maisha ambayo yatakuletea
mafanikio.