Wananchi Waandamana Kupinga Serikali Tripoli Libya

Wananchi wa Libya wamefanya maandamano wakilalamikia hali ngumu ya maisha na kuongezeka umaskini nchini humo. Wananchi hao waliandamana leo mbele ya Kongresi ya Taifa ya nchi hiyo huko Tripoli na kutaka kulipwa fidia familia zote zilizoathirika katika mapinduzi ya mwaka 2011 dhidi ya utawala wa Kanali Muammar Gadafi.

Washiriki katika maandamano hayo wametaka Benki Kuu ya nchi hiyo ishinikizwe ilipe haraka fidia hizo kwa familia ambazo sasa zinateseka na hali ngumu ya maisha.

Maandamano hayo yaliwajumuisha wakazi wa miji ya Misrata, al Zawiya, al Khamis, Zeltan na Sabrata. Washiriki katika maandamano ya leo ya mjini Tripoli Libya wamesema kuwa familia karibu elfu 11 za nchi hiyo ziliathirika vibaya katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakati wa mapinduzi ya tarehe 17 Februari mwaka 2011.