WATU 38 WANAOJIHUSISHA NA UGAIDI WAKAMATWA

 JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam likishirikiana na Mkoa wa Pwani na mikoa mingine ya jiarani limefanikiwa kuwakamata watu 38 wanaojihusisha na vitendo vya kigaidi.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam,Kamanda wa Kanda Maalum ya Kipolisi Dar es Salaam, Suleiman Kova,  amesema kuwa  katika oparesheni ya pamoja na Mkoa wa Pwani kwa kutumia vikosi maalum wamefanikisha kuwakamata  hao nyakati tofauti  na kukutwa na bunduki aina ya SMG 02, SAR 02,Shot gun sita, risasi 310 za SMG/SAR, risasi 37 za G3, risasi 40 za  Shot gun, bomu moja la kurushwa kwa mkono.

Aidha alisema walikamata vifaa vya kutengenezea milipuko sita, Charger sitaza kuhifadhia risasi  na waya wa kuunganisha mabomu na vifaa mbalimbali.Kova alisema  ili kuthibitisha kuwa wahalifu hao si wa kawaida wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za kuficha silaha hizo au wao wenyewe kujificha ili wasigundulike .

Kamanda Kova alidai kuwa kutokana na uwezo, weredi na ushirikiano uliojengeka kati ya jeshi la polisi na raia wema, wahalifu na sialaha hizo waligundulika  wanapojificha na sehemu zilipokuwa zimechimbiwa ardhini kwa kuwekwa makasha mbalimbali.

“Miongoni mwa silaha tulizokamata ni za kituo cha  polisi cha Kimanzichana Wilaya ya Mkuranga, Pwani, na kituo cha polisi cha Ikwiriri, Pwani,   na watuhumiwa wote tunayahifadhi majina yao kwa ajili ya usalama ili kuendelea kutusaidia kuwataja wengine,” alisema Kamanda Kova.