Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe amesema
anamshangaa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.John Magufuli
kuzungumzia masuala ya barabara kila kukicha
huku masuala muhimu akiyaacha katika kampeni zake.
Amesema mgombea huyo amekuwa akizungumzia zaidi mafanikio na
mikakati ya sekta ya ujenzi nchini hususan barabara na kuacha kuizungumzia
nafasi ya urais ambayo ni taasisi kubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam , Kabwe alisema, nchi ya Tanzania ina
changamoto nyingi ambazo zinahitaji kutatuliwa hivyo mikakati ya chama
kinachotarajia kuingia madarakani katika awamu ya tano ni vyema ikawekwa wazi
ili umma ufahamu.
Alisema Magufuli hajaweza kutamka wazi jinsi atakavyoweza
kutatua kero za wananchi katika sekta ya afya, elimu, uchumi na ajira ambazo ni
kikwazo kwa Tanzania
kupiga hatua ya maendeleo.
Aidha, alisema jambo moja angalau lililomfanya avutiwe na
Magufuli ni kuanzishwa kwa mahakama maalum ya kushughulikia mafisadi.
Hata hivyo, alisema hadhani kama
ataweza kulishughulikia suala la ufisadi kwani itamlazimu kuongeza ujenzi wa
magaereza kwa kuwa mafisadi ni wengi.
“Sisi ACT-Wazalendo katika uzinduzi wa kampeni keshokutwa
(jumapili), tumeweka wazi vuipaumbele vyetu ambavyo ni elimu, afya, kutengeneza
mazingira ya uchumi unaozalisha ajira na haki ya kila Mtanzania kuwa na Bima ya
afya na kuwa na hifadhi katika mifuko ya hifadhi ya kijamii,’ alisema.
Alisema chama hicho ndiyo chama pekee ambacho kimeandaa
ajenda hizo katika kampeni za uchaguzi wa mwaka huu, tofauti na CCM ambayo
tayari imekwishaanza kampeni lakini hakuna ajenda zilizopewa vipaumbele.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimekata rufaa kufuatia
mgombea wake wa nafasi ya ubunge katika jimbo la Kinondoni, Kala pina kuambiwa
kuwa hakufikisha vigezo na masharti yaliyowekwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi(NEC).
Alisema kuwa madai ya kuwa mgombea huyo hakupata wadhamini
si ya kweli na chama kimeamua kukata rufaa na wanatarajia NEC itaamua kutenda
haki katika suala hilo .
“Mgombea wetu wanasema hakupata wadhamini hii si kweli
mgombea alipata wadhamini na ushahidi tunao, ni lazima tuwatetee wagombea wetu
ambao wameonyesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali lakini wakakatishwa tamaa
na sababu zisizo za kweli,” alisema.
Chama hicho pia jana kiliendelea kutoa semina ya siku mbili
kwa wagombea nafasi za ubunge ambao watawania nafasi hiyo katika majimbo
tofauti nchini.
Zitto alisema awamu ya kwanza ya mafunzo hayo yametolewa kwa
wabunge 95 huku awamu ya pili ya mafunzo ikiendelea leo kwa wabunge waliobaki.
Chama hicho kinatarajia kuzindua kampeni za uchaguzi Wilaya
ya Temeke, Mbagala Zakheem jijini Dar
es Salaam na baadaye mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa,
Mbeya, Rukwa na Kigoma.