ACT Wazalendo kuanzisha benki kwa watu wa Kigoma

Chama cha ACT Wazalendo kimesema kitashawishi uanzishaji wa Benki ya Kijamii ya Watu wa Kigoma (Kigoma Community Bank) ili kuwawezesha wafanyabiashara, wakulima na vikundi vya ujasiriamali kupata mikopo kwa urahisi na riba nafuu.

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema hayo alipokuwa katika mikutano ya kampeni katika majimbo ya Kigoma mjini na Buhigwe kuwanadi wagombea wa chama hicho ambao walisema kukamilika kwa mpango huo kutainua uchumi na maisha ya watu wengi wa Kigoma na mikoa ya jirani.

“Suala la kuanzisha Benki ya Kijamii kwa Watu wa Kigoma sio jambo la utani, ni mojawapo ya mikakati kumi ya chama chetu cha ACT Wazalendo tunayotaka kuitekeleza endapo tutapata ridhaa ya kushinda urais pamoja na viti vingi vya ubunge,” alisema Zitto.

“Ukienda Mkoa wa Kiliamanjaro utakuta Benki yao, Wilaya ya Mwanga katika Mkoa wa Kilimanjaro, Mbinga mkoani Ruvuma na Mufindi iliyopo Iringa kote huko kuna Benki za Kijamii za maeneo hayo, tunataka na sisi Kigoma tuanzishe Benki yetu ili isaidie katika kukuza mitaji ya biashara za watu ambao wamekuwa wakishindwa kupata mikopo katika benki na taasisi nyingine za kifedha,” aliongeza.

Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa masikini nchini ikiwa ni pamoja na mikoa ya Tabora, Singida na Lindi ambayo licha ya watu wake wengi kuwa na kipato cha chini, imejikuta ikizalisha mazao mengi na kuliingizia taifa fedha za kigeni kama vile tumbaku na kahawa ambayo yamekuwa muhimili mkubwa wa uchumi wa nchi.


Alisema Mkoa wa Kigoma ambao una wakulima, wavuvi, wafanyabiashara na wafugaji unahitaji mtaji wa shilingi bilioni moja ili kuanzisha benki hiyo.