Chama cha Mapinduzi kinasikitishwa na kitendo cha wafuasi wa
vyama vinavyounda UKAWA kupiga mawe na kutupa chupa, baadhi zikiwa na mikojo,
kwenye Ofisi ya CCM Mkoa wa Tanga jana, tarehe 28 Septemba 2015, kabla na baada
ya mkutano wao wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Tangamano, Tanga Mjini.
Tukio la Tanga sio la kwanza. Tarehe 27 Septemba 2015
viongozi wa UKAWA waliwapanga vijana, katika eneo la stendi ya Uyole, mkoani
Mbeya ili wasimamishe msafara wa Mgombea wa Urais wa CCM na kumfanyia vurugu na
kumpigia kelele ili wananchi wasimsikie vizuri. Ingawa Mgombea wetu alifanikiwa
kukabiliana na hali hiyo, tunaamini kwamba huu sio ustaarabu. Washabiki wa CCM
pia wana uwezo wa kupanga na kufanya mambo haya, tena kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Lakini viongozi wa CCM wa ngazi zote wamekuwa wanawahimiza
wasifanye mambo haya kwasababu CCM hatuamini kwamba hiyo ni njia sahihi ya
kuomba ridhaa ya Watanzania kuliongoza taifa letu na pia, kwa kuwa sisi ndio
tuliokabidhiwa na Watanzania nchi hii kuiongoza, tunafahamu dhamana yetu kubwa
ya uongozi wa taifa na ulinzi wa amani ya taifa letu.
Tunawasihi wenzetu wa UKAWA kwamba, katika kipindi hiki cha
kampeni kilichobaki, tufanye kampeni kwa amani ili tumalize uchaguzi kwa amani
na taifa liendelee kuwa na amani baada ya uchaguzi. Wenzetu wa UKAWA
wasitufikishe mahala ambapo washabiki wa CCM watashindwa kuvumilia kuona Chama
chao na viongozi wao wanadhalilishwa.
Tukio la Tanga la Ofisi ya CCM Mkoa wa Tanga kupigwa mawe
limewaudhi na kuwakera wana-CCM na wapenda amani wote wa Tanga. Hata hivyo,
tumewasihi wana-CCM wasilipize kisasi. Chama chetu kina dhamana ya uongozi wa
nchi na ulinzi wa amani ya nchi yetu. Wenzetu dhamana hiyo hawana. Chama chetu
kina uhakika wa kushinda na kushika dola, wenzetu wana uhakika wa kushindwa na
wamekwishakata tamaa.
Tunawapongeza wana-CCM kote nchini kwa utulivu waliouonyesha
katika kipindi chote cha kampeni. Tunawashukuru kwa kubaini na kutoyumbishwa na
propaganda za wenzetu ikiwemo ya Tanga, kwamba mkutano wa Tanga uliahirishwa
kwasababu watu walikuwa wengi. Itakuwa ni mara ya kwanza katika historia kwamba
mkutano wa kampeni unaahirishwa kwasababu ya wingi wa watu. Katika mikutano ya
kampeni, ikiwemo ya CCM, na hata katika sherehe za kitaifa, baadhi ya watu
huzidiwa nguvu na huhudumiwa na wahudumu wa huduma ya kwanza huku mikutano
ikiendelea.
Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa wenzetu kutafuta kisingizio
cha kutofanya mikutano ya kampeni. Mkutano wa kampeni ya UKAWA wa Geita pia
waliuahirisha kwa kisingizio tofauti, kwamba jukwaa na vipaza sauti
havikuandaliwa ingawa aliyetangaza kuahirisha alisimama jukwaani na akasikika
na watu wote. Mabadiliko wanayoyahubiri wenzetu yanaanza na kusema ukweli.
Imefika mahali sasa wenzetu wa UKAWA wawaeleze ukweli Watanzania kuhusu mgombea
wao kushindwa kuhutubia baadhi ya mikutano au kuhutubia kwa dakika 3 kuliko
kuwahadaa kwa kutengeneza matukio na vioja ili kuficha mapungufu ya mgombea
wao.
Tunarudia kuwataka viongozi wa UKAWA kuacha kupanga vurugu,
kuharibu mali
za CCM, na kutukana wana-CCM. Tunarudia kuwataka waache kauli zao za kuibiwa
kura. Kauli hizo ni za kukata tamaa na kuwandaa watu kufanya fujo. Tunadi sera
zetu na wagombea wetu kwa amani ili tuwape Watanzania fursa ya kuchagua kwa
amani ili taifa liendelee kuwa la amani, umoja, utulivu na mshikamano mara
baada ya uchaguzi.
Imetolewa na:
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
29.09.2015