CRDB yatoa msaada wa dawa za kipindupindu Kinondoni

Benki ya CRDB imetoa msaada wa vifaa tiba na dawa za ugonjwa wa kipindupindu kwa Manispaa ya Kinondoni.

Akikabidhi msaada huo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei, alisema benki yake hutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka ili kusadia jamii ikiwamo kutembelea maeneo yenye mahitaji kama vile hospitali, shule na vituo vya watoto yatima.
“Ni dhahiri kuwa wote tunafahamu kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu hususan jijini Dar es Salaam…taarifa za vyombo vya habari zinaeleza kuwa, mpaka sasa Watanzania wenzetu wengi wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huu,” alisema.

Alisema benki yake imeamua kutumia Wiki ya Huduma kwa Wateja kutoa msaada huo wenye thamani ya Sh. milioni 15.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty, alisema msaada huo utanusuru maisha ya Watanzania waliokumbwa na maradhi hayo.


Alisema hadi sasa watu 17 wamepoteza maisha yao  kutokana na maradhi hayo.