Dk Hoseah achaguliwa kuongoza mapambano ya rushwa A.Mashariki

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa TAKUKURU, Dk Edward  Hoseah, amechaguliwa kwa mara nyingine kuwa Rais wa Shirikisho la Mamlaka za Kuzuia na  Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki (East African Association of Anti-Corruption Authorities- EAAACA).

Uchaguzi huo umefanyika leo Jijini Entebe – Uganda, katika Mkutano Mkuu wa nane wa shirikisho hilo ulioanza leo.

Katika taarifa  iliyotolewa na Afisa Uhusiano wa TAKUKURU, Doreen  Kapwani inasema  Dk Hoseah amechaguliwa kwa mara ya pili kushika wadhifa huo kwani yeye ndiye aliyekuwa rais wa kwanza wa shirikisho hilo lililoanzishwa mwaka 2007”.

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kwake, Dk Hoseah amesema katika kipindi cha uongozi wake kama rais wa EAAACA (2015 -2017) atatoa kipaumbele  katika  kuweka mikakati michache inayotekelezeka ikiwemo kufanya tafiti za kuziba mianya ya rushwa katika mifumo mbalimbali ya taasisi katika za nchi za Afrika Mashariki.

Pia aliongeza kuwa atamarisha uhusiano kati ya taasisi za kuzuia na kupambana na rushwa Afrika Mashariki na kuongeza jitihada za kuhakikisha EAAACA inajumuishwa katika Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (East African Community).


Shirikisho hilo linalojumuisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, liliundwa rasmi mwaka 2007, ambapo viongozi wa TAKUKURU (Tanzania), IG (Uganda) na KACC (Kenya) - ambao ndio waanzilishi, walisaini Azimio la kuwa na Ushirikiano wa Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki.