Dk Shein ahofia kauli za CUF

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Ali Mohamed Shein amesema kauli zinazotolewa na viongozi wa CUF zina dalili ya kuvuruga Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.

Akizungumza katika kampeni zilizofanyika kwenye Uwanja wa Mkokoto, Mkoa wa Kaskazini Unguja jana, Dk Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, alisema viongozi hao wanaeneza lugha za vitisho kuwa awamu hii CCM lazima iachie madaraka na kuikabidhi CUF.

“Kuna utaratibu wa kuiondoa Serikali kupitia uchaguzi na siyo vitisho. Lugha za kutisha nazijua, hivyo viongozi wa CUF wafanye kampeni za kistaarabu,” alisema Dk Shein na kuongeza kuwa CCM na CUF vipo ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Ismail Jussa alisema hawana mpango wa kufanya vurugu kwenye Uchaguzi Mkuu badala yake wana taarifa kuwa CCM imejiandaa kufanya vurugu.

“Nimeandaa waraka wenye pointi 12 za namna CCM wanavyojiandaa kufanya vurugu kwenye Uchaguzi Mkuu,” alidai Jussa.

Dk Shein katika mkutano huo aliwaambia wananchi kuwa ataendelea kulinda amani kama alivyofanya katika miaka mitano iliyopita.

Alisema vikosi vya kulinda amani vitapatiwa vifaa vya kisasa ili wafanye kazi kwa ufanisi zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alisema CCM ina taarifa kuwa CUF wanapanga kufanya vurugu Oktoba 24, 25 na 26, huku akionya wasifanye hivyo kwa kuwa vyombo vya dola vitawachukulia hatua.


“Wasiwaachie wafuasi wao kufanya vurugu, vyombo vya dola vipo imara, wasije wakajilaumu. Wasijaribu kufanya maandamano siku hiyo,” alionya Balozi Idd.