Facebook Sasa Kuja na Kitufe cha ‘Dislike’

Kama umekuwa ukitembelea ukurasa wako wa Facebook, kuna wakati unajiuliza kwa nini kuna kitufe cha kupenda tu (Like) wakati hakuna kitufe cha kuchukia (Dislike). Facebook wamekuwa wakijiuliza swali kama hilo pia, na sasa wanakuletea kitufe hicho katika ukurasa wako.

“Watu wengi wamekuwa wakiulizia kuhusu kitufe cha ‘Dislike’ (Chuki) kwa miaka mingi, na pengine mamia ya watu wanauliza kuhusu hili. Hivyo leo ni siku ya kipekee kwani ni siku ambayo natangaza kuwa tunalishughulikia hilo, na punde tu tutaweka kitufe hicho kwa ajili ya majaribio.” Anaelezea Mark Zuckerberg, mmiliki wa mtandao wa Facebook.

Zuckerberg, alieleza hayo wakati wa muda wa maswali na majibu huko Califonia siku ya Jumanne amesema kitufe hicho hakijakusudiwa kuwa sehemu ya kuchagua kipi ni kizuri au kibaya, au sehemu ya kupiga kura kuhusu posti za watu.

Badala yake, amesema kitufe cha chuki kimeweka kwa ajili ya posti ambazo zinahusisha huzuni ambapo watu hutaka kitufe cha chuki kuonyesha kuhuzunishwa na posti badala ya kuipenda.

 “Kitufe cha chuki kimewekwa kwa ajili ya kuonyesha huruma kwa marafiki, si kwa ajili ya kuonyesha kumchukia rafiki. Wakati mwingine, rafiki huweza kuposti kuhusu msiba wa ndugu yake, na inakuwa vigumu kupenda posti kama hiyo”. Alifafanua Mark.

Zuckerberg ameeleza kutatanishwa sana na kitufe cha chuki, na kuelezea kuwa ndio sababu kubwa ya kucheleweshwa kwake Facebook, huku akieleza kuwa Facebook ni sehemu ya marafiki na si sehemu ya kueneza chuki. Hivyo kitufe cha ‘Chuki” kitafanyiwa majaribio ya mwanzo kabda ya kuruhusiwa kutumika kuwafariji marafiki, na si kuwachukia.

Zuckerberg aliwahi kukaririwa kusema kuwa, Facebook kamwe wasingeweza kuweka kitufe cha Chuki (Dislike), lakini kutokana na kushindwa kujua hisia za watumiaji zaidi ya bilioni 1.5, amekuwa akiamini wote hawana hsia za kupenda pekee.

“Kama unaelezea kitu cha huzuni, haitakuwa kitu kizuri kupenda posti yako. Lakini marafiki zako watahitaji kitu kukuonyesha kuwa wanaelewa hisia zako na wanakufariji.


Tuendelee kusubiri ujio wa kitufe hicho ila kwa kiasi kikubwa kuna uwezokano wa kuja kitofauti kabisa. Kuna uwezekano wa kitufe hicho kuja katika mfumo wa kutoa pole au kuonesha hisia za huzuni kwa kilichoandikwa na rafiki yako badala ya kuonesha chuki n.k. Tuendelee kusubiri.