Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Moshi Mjini, Zakaria
Laizer amepewa likizo ya lazima ya siku 30, akituhumiwa kumuunga mkono mgombea
urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Kiini cha kupewa likizo hiyo kinatokana na kukutwa akipata
chakula na viongozi wawili wa zamani wa CCM katika mikoa ya Kilimanjaro na
Arusha, ambao sasa wamehamia Chadema.
Viongozi hao ni katibu wa zamani wa Itikadi na Uenezi wa
mkoa wa Arusha, Issack Kapriano maarufu Kadogoo na Katibu wa zamani wa Uchumi
na Fedha mkoa Kilimanjaro, Paul Matemu.
Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi, Loti Ole Nesele
alilithibitishia gazeti hili jana kuwa Laizer kapewa likizo hadi baada ya
uchaguzi.
“Miye sipo Moshi niko Babati, lakini ni kweli alipewa barua
hiyo ya likizo wiki iliyopita, ukiniuliza sababu sitakwambia kwa sababu ni siri
za mtumishi na ofisi,” alisema.
Hata hivyo, chanzo cha habari cha uhakika kinasema, Kadogoo
ambaye ana undugu na Laizer alimpigia simu ndugu yake huyo akimjulisha kuwa
angepita Moshi akienda Mwanga, hivyo amsaidie kumwekea oda ya chakula, naye
akafanya hivyo katika mgahawa wa East African ambapo walikutwa na kiongozi mmoja
wa CCM.
Mtu aliye karibu na Kadogoo, alisema katibu huyo alimpigia
simu Matemu ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi ili ajumuike nao chakula cha
jioni.
Taarifa hizo zinadai siku iliyofuata, Laizer aliitwa na
kuhojiwa na viongozi wa CCM, lakini akajitetea kuwa Kadogoo ni mjomba wake na
asingeweza kumtenga kwa vile amehamia Chadema.
Laizer ni miongoni mwa wana- CCM waliokuwa wakimuunga mkono
Lowassa wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.
Kutokana na tuhuma za kuendelea kushirikiana na mgombea huyo
wa Ukawa, viongozi hao walipendekeza kwa uongozi wa mkoa wa Jumuiya hiyo umpe
likizo ya lazima Laizer kwa siku 30, ili arejee baada ya Uchaguzi Mkuu
kumalizika.
Laizer alipoulizwa kuhusu likizo hiyo alisema hawezi
kuzungumzia suala hilo
lakini mwenzake, Matemu licha ya kukiri kukaa meza moja na Laizer siku hiyo,
alieleza kushangazwa na likizo akisema mjumuiko walioufanya haukuwa na ajenda
yoyote ya kisiasa.
“Nimejiuliza maswali mengi lakini sipati majibu. Kwamba CCM
imefika mahali inataka wana CCM wasichanganyikane na wafuasi wa vyama vingine.
CCM wanataka kufanya siasa ni uadui?” alihoji.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM mkoa Kilimanjaro,
Festo Kilawe, alipoulizwa kuhusu sakata hilo ,
aliomba aulizwe katibu wa jumuiya hiyo mkoa wa Kilimanjaro, Robert Chilamato.
Hata hivyo, Chilamato ambaye ndiye aliyesaini barua ya
likizo hiyo, alitaka watafutwe viongozi wa wilaya wa jumuiya hiyo. “Hilo jambo waulizwe
viongozi wa wilaya (wa jumuiya) kwa vile mimi ni kiongozi wa ngazi ya mkoa,”
alidai Chilamato.