Habarini ndugu zangu wakulima na wadau wote wa Kilimo.
Nilikwisha wahi andika juu ya Kilimo bora cha Uyoga, na kueleza kwa kina ni jinsi
gani mkulima anaweza kunufaika na kilimo hiki. Lakini basi leo ningependa
nifundishe juu ya Kilimo rahisi kabisa cha zao hili la Uyoga ambapo hata
mkulima mdogo kabisa huko kijijini anaweza kumudu katika kilimo hiki.
Namna ya kuotesha
Uyoga.
Kabla ya kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa
ambalo litazuia jua, mvua na vumbi. Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu
inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa
Uyoga. Mkulima wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza .
Hatua muhimu katika kuotesha Uyoga baada ya kupata mbegu ni kama ifuatavyo:
. Kusanya masalia ya mazao kama
vile mabua, majani ya mpunga, ngano, Pumba za mpunga au mahindi, masalia ya
miwa baada ya kukamua n.k
Vitu hivi hutumika kama mali ghafi kwa kuoteshea Uyoga.
. Mabua, Majani ya Mpunga au Migomba yakatwe kwa urefu
usiozidi sentimeta 6, au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.
. Loweka mali
ghafi kwenye maji ya kawaida kwa muda wa siku nzima ( saa 24).
. Kisha yachemshwe kwa muda wa saa 2 ili kuua vijidudu
pamoja na vimelea vilivyomo.
. Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye kichanja
kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu.
. Kisha jaza mali
ghafi hii katika mifuko ya nailoni tayari kwa kupanda mbegu.
Namna ya kupanda.
Kuna aina mbili za
upandaji;
AINA YA KWANZA
Chukua mfuko wa nailoni, weka tabaka ya mali ghafi ya kuoteshea kiasi
katika mfuko halafu tawanya mbegu juu yake.
Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya
kuoteshea na kuweka mbegu juu yake.
Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifikie ujazo wa
robo tatu ya mfuko.
NB: Tabaka la mwisho la juu lazima liwe la vioteshea.
AINA YA PILI
Changanya mali
ghafi ya kuoteshea ( baada ya kuchemsha na kupoa) na mbegu ya uyoga katika
uwiano wa 1:25 ( mbegu : mali
ghafi ya kuoteshea).
Kwa uyoga aina ya Mamama ( Pleurotus spp), kisha
mchanganyiko huu ujazwe katika mifuko ya nailoni. Mifuko hii iwe ya ukubwa wa
sm 20 kwa sm 40 ambamo unaweza kujaza kilo 1-1.5 ya mali ghafi ya kutosha.
Katika njia zote mbili, funga mifuko na toboa matundu kwenye
mifuko yenye kipenyo cha sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko.
Zingatia:
(i) Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya
mifuko.
Uyoga ni Kiumbe hai, hivyo unahitaji kupumua.
(ii) Ukishanunua mbegu, kama
hupandi kwa muda huo, hifadhi kwenye jokofu. Kama
huna jokofu, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu. Mbegu za uyoga zinaweza
kuota vizuri hata zikikaa nje ya jokofu kwa siku mbili.
(iii) Waweza kutumia chupa moja yenye ujazo wa mililita 300
kwenye kilo 15 za mali
ghafi ya kupteshea. Hakikisha unamaliza mbegu yote kwenye chupa kwani ikibaki
itapata maambukizo ya vimelea.
(iv) Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo
siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea. Vingine na hivyo haifai
kupandwa.
Makala hii imeandaliwa na kuandikwa na Marcodenis E.
Misungwi, Agriculture Extension Officer at Mbozi District Council.
MATUNZO YA ZAO LA
UYOGA.
Weka mifuko kwenye chumba cha giza . Kwa mkulima wa kawaida waweza kutumia
kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza .
Acha mifuko humo kwa muda wa siku 14-21 bila kufunua ili
ukungu mweupe uweze kutanda vizuri.
Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya
kuoteshea, hamishia kwenye chumba cha mwanga na hewa ya kutosha kisichopigwa
jua.
Katika chumba chenye mwanga. Mifuko inaweza kuwekwa kwenye
meza, chanja ya waya au miti. Mifuko pia inaweza kuning'inizwa kwenye kamba.
NB: Unaweza kunyunyizia maji juu ya mifuko yaliyochemshwa na
kupoa, mara tatu au zaidi kwa siku.
Tahadhari:
Usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yanaweza kuozesha uyoga.
Aina nyingi za uyoga huanza kutoa vichwa siku 2-3 baada ya kuwekwa
kwenye mwanga.
UVUNAJI WA UYOGA.
Uyoga huwa tayari kuvunwa siku tatu baada ya vichwa
kuonekana.
Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la
uyoga, kisha zungusha hadi uyoga ung'oke.
Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwa kubakiza
shina huzuia uyoga mwingine kutokea.