Kipindupindu chaingia Morogoro, mmoja afariki dunia

Wakazi wa Kata ya Mindu Manispaa ya Morogoro wamekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu  ambapo hadi sasa mtu mmoja ameripotiwa kufa na hivyo kuzua hofu kwa wakazi  wa eneo hilo na manispaa kwa ujumla.

Akizungumza na Mwananchi  Katika Kambi maalumu ya wagonjwa wa Kipindupindu,  Afisa  Afya wa Manispaa ya Morogoro, Gabriel Malisa  alimtaja aliyefariki kuwa ni  Mkolole  Shomari (65).

Amesema kuwa mtu huyo alifariki nyumbani kwake maeneo ya Mindu  baada ya  majirani zake ambao wametokea Dar es salam  kuwa na ugonjwa huo licha ya kuwa walianza kutibiwa Amesema kuwa baada ya muda mfupi  marehemu alianzwa na dalili za ugonjwa huo za kuharisha na kutapika  bila kuchukua tahadhari  hatimaye kupoteza maisha.

Hivyo Afisa afya huyo aliwatahazalisha wakazi wa manispaa ya Morogoro kuwa makini na ugonjwa huo na kutoa taarifa pindi tu wanapo muona mtu ana dalili za ugonjwa huo ili aweze kupatiwa matibabu haraka Katika eneo husika.


Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa kata ya mindu Abed Ibrahim na Chales Ollynkute wamesema kuwa licha ya kuwa ugonjwa huo umeingia Katika manispaa ya Morogoro bado wakazi wake hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na kujikinga na ugonjwa huo ambao umekuwa ukipoteza maisha ya watu  kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha.