Wakazi 11 wa Manispaa ya Singida, wamelazwa kwenye kambi ya
Mandewa iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa kipindupindu, wakihofiwa kuugua
ugonjwa huo.
Tayari watatu kati yao
wamethibitika kuwa na kipindupindu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana,
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Singida, Dk John Mwombeki alisema mgonjwa wa kwanza
alipokelewa Septemba 25, mwaka huu na kulazwa katika hospitali ya mkoa.
Alisema mgonjwa huyo alitokea jijini Dar es Salam, Septemba
24.
“Alipolazwa
hospitalini na kuchukuliwa vipimo, aligundulika kuwa na kipindupindu na
kuanzishiwa matibabu, ambapo kwa sasa anaendelea vizuri huko kwenye kambi,”
alisema Dk Mwombeki.
Mganga huyo alisema mgonjwa mwingine alitokea Kijiji cha
Ilongero katika Jimbo la Singida Kaskazini na wa tatu alitokea Mtaa wa Majengo
Singida mjini.
Dk Mwombeki alisema wagonjwa wengi waliolazwa katika kambi
hiyo wanaharisha damu na kutapika.
Pia alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha wakazi wa manispaa
hiyo kuwa wakiona dalili za ugonjwa huo ikiwamo, kuharisha wafike haraka katika
vituo vya afya waweze kupata huduma ya vipimo kujua kama
tatizo ni ugonjwa huo.
“Tumeshawatangazia
kuwa wahakakikishe wanatumia majisafi na salama, na yachemshwe kwanza kabla ya
kutumika. Vyakula hali kadhalaika viliwe vingali vya moto,” alifafanua.
Wakati huohuo, mganga huyo alitoa wito kwa wamiliki wa
mabasi, hasa ya masafa marefu wahakikishe wanayafanyia usafi wa kutosha kwenye
viti vya abiria ili kuondoa uwezekano wa abiria wengine kuambukizwa
kipindupindu.
Alisema kuna uwezekano abiria wenye vimelea vya ugonjwa huo
wakaviacha kwenye viti vya mabasi.