WATU wawili wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa
Kipindupindu mkoani wilayani Kongwa, Dodoma .
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Mganga Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma , Dk.
Ezekiel Mpuya. Dk. Mpuya amesema hivi karibuni walipokea mgonjwa mmoja wa
kipindupindu kutoka katika kijiji cha Mkoka kata ya Mkoka wilayani Kongwa.
“Hapo kulikuwa na
familia moja iliyokuwa mkoa wa Morogoro kwenye eneo ambalo linasadikiwa kuwa na
ugonjwa wa kipindupindu, alisafiri kuja eneo la Mkoka bila ya wao kufahamu
mtoto alianza kuharisha.
“Lakini alipopelekwa
kwenye kituo cha afya cha Mkoka na kuchukuliwa vipimo walibaini kwamba ni
ugonjwa wa kipindupindu,” amesema.
Aidha, amesema hadi juzi kulikuwa na wagonjwa saba kwenye
kituo hicho ambapo wawili walifariki dunia.
Hata hivyo, amesema katika kijiji hicho cha Mkoka kuna
mwanakijiji mmoja naye alisafiri kuja Manispaa ya Dodoma ambapo alionekana kuwa na dalili za
ugonjwa huo.
“Alipoona dalili hizo
aliamua kwenda kwenye kituo cha Afya cha Makole na kuchukuliwa vipimo, ingawa
vipimo vimeonyesha kuwa hana dalili za kuhara lakini sisi tunamashaka na
tunaendelea kumuhudumia,” amesema.
Aidha, amewaasa wananchi kuwa waangalifu ikiwa ni pamoja na
kuchukua tahadhari kwa kuwa ugonjwa wa kipindupindu unatokana na kula kinyesi.
“Wanatakiwa kunawa
mikono na sabuni wanapotoka chooni na kabla ya kula, na vyakula wanavyokula
viwe visafi,” amesema.
Amesema walipotembelea katika kijiji cha Mkoka waligundua
kuwa wakazi wengi wa eneo hilo
hawana vyoo.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk. Donan Mmbano amesema mpaka sasa ni mikoa mitano ndiyo iliyoathirika
na Ugonjwa wa Kipindupindu.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es
Salaam , Dodoma ,
Kilimanjaro, Iringa na Morogoro.
