MAGUFULI Nitakufa na Wezi wa Dawa za Hospitali

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewataka watumishi wa Bohari ya Dawa (MSD), kukaa mguu sawa kwa sababu hatakubali kusikia hospitali za serikali zikikosa dawa kama ilivyo sasa.

Dk. Magufuli alisema inashangaza kuona wananchi wanateseka kwa kukosa dawa kwenye hospitali za serikali na wagonjwa kuandikiwa kwenda kununua dawa hizo kwenye mduka binafsi.

Alitoa onyo hilo jana wilayani Kilindi, mkoani Tanga wakati akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni.

“Hawa wanaohusika na kusambaza madawa wakae mguu sawa maana serikali ya Magufuli haitakubali kuona wananchi wanaendelea kunyanyasika kwa ukosafu wa dawa wakati kwenye maduka binafsi zipo,” alisema Dk. Magufuli na kushangiliwa na wananchi hao.

DK. Magufuli alisema hajaomba nafasi ya urais kufanya majaribio, hivyo watumishi wazembe serikalini wanaokwamisha huduma za maendeleo ya Watanzania wanapaswa kujitazama upya.

Aidha, Dk. Magufuli alisema Tanzania si maskini kwani ina raslimali nyingi isipokuwa mafisadi wachache na wengine wakiwa serikalini ndio wameifikisha nchi pabaya kwa kutumia nafasi zao vibaya.

“Nipeni urais muone namna nitakavyowashughulikia hawa mafisadi, hawa ndiyo wamesababisha wananchi wengine kuichukia serikali kwa kuwa wamekuwa wakitumia fedha zao kuwanyanyasa wananchi wa hali ya chini ambao wanakosa huduma hospitalini,” alisema Dk. Magufuli.

Mgombea huyo alisema nafasi ya urais inamtosha, hivyo wasihangaike na wagombea wa vyama vingine ambao alisema wamekuwa wakitoa ahadi ambazo hawana uwezo wa kuzitekeleza.

“Nafasi ya urais inanitosha kwa sababu lengo langu ni kuwatumikia Watanzania, najua hapa Songe mnahitaji lami, nimeweza kujenga kilomita nyingi nchini na madaraja mengi, siwezi kushindwa kilomita tano za lami  hapa Songe,” alisema.

Katika hatua nyingine, msafara wa Dk. Magufuli uliingia mkoani Tanga kutoka Morogoro kwa kishindo kutokana na mapokezi makubwa aliyoyapata kutoka kwa wanachama wa CCM na wananchi wa mkoa huo.

Msafara wa mgombea huyo ambao ulikuwa ukitokea mkoani Morogoro, ulisimama katika vituo zaidi ya 14 ukiwa njiani kuelekea wilaya ya Kilindi na Handeni mkoani humo ambapo alikuwa akizungumza na wananchi waliokuwa wamefurika barabarani wakimsubiri.

Dk. Magufuli alilazimika kusimama njiani na kuzungumza na wananchi hao na kuwanadi wagombea wa udiwani wa maeneo husika kutoka CCM ambao walikuwa barabarani na wananchi wakimsubiri kwa muda mrefu.


Mgombea huyo alielezea kufurahishwa na mapokezi hayo ya aina yake aliyopata mkoani humo na kuahidi kuwa ameondoka na deni na njia pekee ya kuwalipa wananchi hao ni kuhakikisha anatatua kero zao.