Magufuli : Nitawafunga mafisadi kwa makufuli

Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amewataka Watanzania wampe kura ili akiingia Ikulu akawafunge mafisadi kwa makufuli.

Dk Magufuli alitoa kauli hiyo jana katika Kijiji cha Mvumi Mission alipokuwa akihutubia umati wa wananchi waliojitokeza kumsikiliza na kusisitiza kuwa serikali atakayoiongoza haitakuwa na mchezo wala uonevu kwa wanyonge.

“Nipeni kura za kutosha ili nikiwa rais, niwafunge mafisadi kwa makufuli, hapa ni kazi tu,” alisisitiza Dk Magufuli.

Huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza katika Uwanja wa Mvumi, Dk Magufuli alisema akiingia madarakani atasimamia na kuhakikisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Dodoma hadi Mvumi Mission unakamilika.

Aliwatupia vijembe baadhi ya wagombea kutoka vyama vingine kwamba wamekuwa na tabia ya kubeza maendeleo yaliyofanywa na CCM wakati wanajua na wanaona.

Awakutanisha Lusinde, Malecela
Mkutano huo wa Dk Magufuli uliwakutanisha mahasimu wawili kisiasa, Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela na mgombea ubunge wa Mtera, Livingstone Lusinde ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawakai meza moja.

Akizungumza jukwaani, Lusinde alimfananisha Malecela na watu wenye uvumilivu lakini pia akasema ana afya nzuri kama ilivyo kwa wastaafu wengine akiwawamo; Joseph Warioba, Dk Salim Ahmed Salim na hata Rais Jakaya Kikwete ambao alisema bado wanaweza kusimama kwenye majukwaa kwa muda mrefu.

Lusinde alimshukia Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kuwa hana shukurani na kwamba kama ameshindwa kushiba kipindi akiwa waziri mkuu alichokaa miaka 10, hawezi kushiba kwa sasa.

“Mimi ninaomba Magufuli ukiapishwa tu, tusaidie watu wa Mtera. Tuna njaa kutokana na mvua ambazo hazikunyesha, tusaidie maji na mawasiliano katika maeneo yetu, ujenzi wa barabara ya lami Mvumi – Dodoma pamoja na kuiona kwa karibu wilaya yetu ni kubwa hebu igaweni,” alisema Lusinde.

Malecela ambaye ni makamu mwenyekiti wa CCM mstaafu, aliwataka Watanzania kuichagua CCM ili iweze kuwapelekea maendeleo.

Aliwauliza wananchi wa Mtera iwapo wangekuwa tayari kuwabeba Ukawa migongoni, nao wakaitikia kuwa hawako tayari.

Alisema kura za ushindi kwa CCM zinatakiwa kufanyika nyumba kwa nyumba ili ushindi uwe mkubwa na kuwabeza wapinzani wanaosema chama hicho hakijafanya kitu wakati kuna barabara za lami kutoka Dar es Salaam hadi Sumbawanga, vitu ambavyo havikuwapo.

Leo, Dk Magufuli atafanya ziara katika majimbo ya Mpwapwa Mjini, Kongwa na kuhitimisha katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Aahidi barabara Isimani
Akiwa Iringa, Dk Magufuli aliwaahidi wakazi wa Jimbo la Isimani kuwa akichaguliwa, atajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Izazi – Pawaga - Mlowa mpaka Hifadhi ya Mbuga ya Ruaha.

Pia, alisema atawapatia wafugaji maeneo ya malisho na kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, uimarishaji miundombinu ya umwagiliaji na uboreshaji wa Kituo cha afya Tarafa ya Pawaga ili kiwe katika kiwango cha hospitali.

Dk Magufuli aliwaeleza wananchi kuwa akichaguliwa watarajie serikali ya awamu ya tano kuwa ya wachapakazi.

Akimnadi mgombea ubunge wa Isimani kupitia CCM, William Lukuvi alisema, anamfahamu vyema kwa kuwa amekuwa naye katika awamu nyingi serikalini na ni mchapakazi, hivyo atashirikiana naye kutatua changamoto zilizopo.

Katika Kijiji cha Migoli alikofanya mkutano wake wa mwisho mkoani Dodoma, Dk Magufuli alikumbushia ahadi ya Sh50 milioni kwa kila kijiji kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana na wanawake.

Alisema ana uzoefu serikalini, hivyo anajua fedha zitatoka wapi na atahakikisha kila kijiji au kitongoji kinapata mgawo huo.

CCM yalalamikia Ukawa
Katika hatua nyingine, CCM imelalamikia vitendo vya wafuasi wa Ukawa, kufanya vurugu katika mikutano na misafara ya mgombea wake, Dk Magufuli kwa kuwa hali hiyo inahatarisha uvunjifu wa amani.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, iliyosainiwa na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni, January Makamba jana, CCM ilidai viongozi wa Ukawa waliwapanga vijana wao maeneo ya Stendi ya Uyole na kumpigia kelele Dk Magufuli ili asisikike wakati mkoani Tanga walipiga mawe ofisi za mkoa.

“Wafuasi wa CCM wana uwezo wa kupanga na kufanya hayo, lakini tumekuwa tukihimiza amani na kufanya hivyo si njia sahihi ya kuomba ridhaa kwa wananchi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

January alisema kuwa CCM inawasihi Ukawa kufanya kampeni za amani ili kumaliza mchakato kwa amani.


“Tukio la hivi karibuni la kupigwa mawe ofisi za CCM Tanga na kufanya vurugu, Uyole zimekera,” alisema.