UKATILI! Mwalimu Nelson Andrew (23), amevamiwa na watu
wanaodaiwa kuwa ni vibaka na kumkata kwa kisu koromeo katika jaribio la kumtaka
awape fedha la sivyo wangemuua.
Mwalimu Nelson Andrew akiwa na jeraha shingoni baada ya
kujeruhiwa.
Akizungumza na Uwazi hivi karibuni, kaka wa mwalimu huyo,
Andes Enock alisema tukio hilo
lilijiri saa nane mchana wa Septemba 10, mwaka huu, wakati yeye na mjeruhiwa
huyo wakipitisha biashara ya vyombo hatua chache kutoka kwenye nyumba
wanayoishi.
“Tulikuwa na mwalimu, mimi nilikuwa mbele yake huku
tunaongea lakini kila nilipoongea hakuwa akinijibu.
ilipoangalia nyuma ndipo nikaona amepigwa kabali na kundi la
vijana zaidi ya wanane huku amepitishiwa kisu shingoni na damu zikimtoka
chapachapa. Alikabwa kiasi cha kushindwa kupiga kelele. Nilipouliza kuna nini,
wale wahalifu walimwachia na kukimbia.
“Mwalimu alidondoka chini
huku akizidi kutokwa damu nyingi. Nilitafuta usafiri na kumpeleka Kituo cha
Polisi cha Mwinyijuma ambapo tulipewa PF 3 kisha tukamkimbiza Hospitali ya
Mwananyamala ambapo madaktari walisema tatizo ni kubwa hivyo kumpeleka
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Alifanyiwa uchunguzi
na ikabainika kwamba alikuwa amekatwa koromeo. Alikuwa akipumua kwa shida hali
iliyosababisha afanyiwe upasuaji na kulazwa kwa siku tano.“Mpaka sasa anapumua
kwa shida ndiyo maana hospitali walimtoboa tundu kwenye koromeo, anashindwa kula,
anakunywa uji tu tena kwa shida.
“Mdogo wangu ni mkazi
wa Kijiji cha Nyanganga, wilayani Uvinza, Kigoma. Baada ya kumaliza masomo Chuo
cha Ualimu Ndala, Tabora alikuja hapa kwangu akisubiri kupangiwa kazi. Niliona
tusaidiane katika biashara ya kutembeza vyombo mitaani lakini kwa bahati mbaya
akavamiwa na kujeruhiwa,” alisema Andes .
Hata hivyo, hali ya mwalimu huyo bado ni mbaya na anahitaji
matibabu ya karibu lakini kinachowapiga chenga ni gharama kwa vile alikuwa
hajaajiriwa.Hivyo kwa yeyote anayependa kumsaidia anaweza kutumia namba 0676
416378 au 0759 538451.