Kocha msaidizi wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Hemmed
Morocco ametangaza kikosi cha wachezaji 24 watakaocheza na Malawi huku akiwaengua wachezaji watano
waliokuwapo kwenye kikosi kilichoivaa Nigeria mwezi uliopita.
Wachezaji walioenguliwa kwenye kikosi hicho ni Abdi Banda
(Simba), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Abdurahman Mbambi (Mafunzo), Ramadhan
Singano na Ame Ally.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Morocco alisema kikosi hicho
kitaingia kambini Oktoba Mosi tayari kujiandaa na mchezo huo wa mtoano wa
kuwania kupangwa kwenye makundi ya kugombea tiketi ya kucheza Fainali za Kombe
la Dunia 2018 nchini Urusi.
Iwapo Stars itafanikiwa kuitoa Malawi ,
Tanzania itaingia kwenye
raundi ya pili ya kufuzu ambako itamenyana na Algeria . Ikifuzu mtihani wa Algeria , Tanzania itafanikiwa kupangwa
kwenye kundi la kuwania tiketi ya kwenda Russia 2018.
Kutokana na kuwa chini kwenye viwango vya Fifa. Tanzania imelazimika kuanza hatua ya awali kwa
kumenyana na Malawi ,
Jumatano ijayo Oktoba 7.
Morocco aliwataja wachezaji ambao wataingia kambini kuivaa
Malawi kuwa ni makipa Ally Mustapha ‘Barthez’, Aishi Manula na Said Mohamed
wakati walinzi ni Shomari Kapombe, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Hassan Isihaka,
Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani.
Kwa upande wa viungo watakaounda kikosi hicho ni Frank
Domayo, Salum Telela, Said Ndemla, Deus Kaseke, Mudathir Yahya, na Farid Musa
huku washambuliaji wakiwa John Bocco, Rashid Mandawa, Ibrahim Hajib na
wachezaji wa kimataifa waliounganishwa kwenye kikosi hicho ni Mbwana Samatta,
Thomas Ulimwengu (TP Mazembe- DR Congo) na Mrisho Ngassa (Free State – Afrika
Kusini).
Katika hatua nyingine, Morocco amemshauri Mwinyi Kazimoto
kuwa umri wake bado ni mdogo kutangaza kuacha kulitumikia taifa na
anachokifanya ni kujimaliza.