Polisi Arusha yaua raia wa ndani na nje watuhumiwa wa ujambazi

Watu wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliuawa na askari Polisi wakati wa mapambano ya majibizano ya risasi usiku wa tarehe 17.09.2015 saa 3:30 maeneo ya Chekereni mpakani mwa wilaya ya Arumeru na halmashauri ya Jiji la Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alielezea mazingira ya tukio hilo kuwa jeshi hilo lilipokea taarifa za Kiintelejensia juu ya kuwepo kwa kundi la majambazi lililotaka kufanya uvamizi na uporaji ndani ya jiji la Arusha. 

“Tulipata taarifa tangu Agosti 19 mwaka huu kuwa kutakuwepo kundi la majambazi toka nchini Kenya ambalo wangeshirikiana na wengine wa hapa nchini kwa nia ya kufanya uhalifu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo taasisi za fedha”. Alisema Sabas.

Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa hiyo waliendelea na ufuatiliaji na kufanikiwa kukamata kwa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Sixtus Alfredy Ngowi (51) Mtanzania, Mkazi wa Ngulelo katika jiji hilo juu ya kushirikiana na majambazi wenzake wanaodaiwa toka nchini Kenya ambao hufanya matukio mbalimbali ya kiuhalifu hapa nchini.

Baadhi ya matukio ambayo majambazi hayo yameyafanywa ni pamoja na tukio la uporaji wa fedha zaidi ya dola 2,000,000 lilitokea jijini Dar es salaam mwaka 2005 kwenye Kampuni ya Security Group 4.

Mbali na tukio hilo pia mwaka 2002 wanadaiwa kuhusika na tukio la uvamizi wa Benki ya NBC tawi la Moshi mkoani Kilimanjaro huku Mwaka 2014 jambazi huyo amewahi pia kushtakiwa nchini Kenya kwa matukio ya uhalifu katika Mahakama ya Mlimani Law Court iliyopo jijini Nairobi lakini baadae aliachiwa huru.

Alizidi kukiri kuhusika katika matukio ya ujambazi huku akishirikiana na wenzake katika matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika jiji la Arusha ambalo lilikuwa linawalenga wafanyabiashara wakubwa wa Madini ya Tanzanite na Hoteli za Kitalii.

Miongoni mwa tukio walilolifanya ni kumjeruhi mfanyabiashara wa madini aitwaye Mathius Manga ambaye alipigwa kwa risasi kwenye ubavu wa kulia.

Kamanda Sabas alisema kwamba mara baada ya kuridhishwa na mahojiano baadae jambazi huyo alikubali kushirikiana na Polisi ili aweze kufanikisha juu ya upatikanaji wa wenzake ambao siku ya jana walipanga kuvamia katika duka la kubadilishia fedha liitwalo Sanya lililopo jijini Arusha.

Walipokuwa wanaelekea kwenye eneo la tukio akiwa anaongozana na askari Polisi kwa nia ya kufanikisha kuwapata majamabzi wengine, mara tu baada ya kufika kabla hawajawakamata majambazi hao ambao walikuwa kwenye gari aina ya Noah rangi ya silver yenye namba za usajili T. 981 AVK walishtuka na kuanza kulishambulia gari lililokuwa na askari Polisi na kumjeruhi mwenzao Sixtus Alfedy Ngowi ambaye alifariki muda mfupi wakati akiwa njiani kupelekwa hospitali.



Mara baada ya kuona hivyo, Polisi nao walijibu mapigo na kufanikiwa kuwaua majambazi watatu huku wengine wakifanikiwa kukimbia. Katika upekuzi kila mmoja alikutwa na bastola pamoja na risasi. Pia walikuta mabegi matatu meusi ambapo ndani yake kulikuwa na bunduki mbili aina ya AK 47 zenye namba 83 LG 3953 56-1 na nyingine yenye maandishi ya kirusi pamoja na SMG moja yenye namba 56-1 28038394.

Bastola ambazo zilikutwa toka kwa majambazi hao zilikuwa na namba CZ 75 Compact Luger-9mm namba A. 269206, CZ 85 B Luger 9mm namba 051967 na Chines Pistol namba 967741. Pia zilipatikana magazine nne tupu za SMG, risasi 85 za SMG/AK 47 na risasi 28 za bastola.
Mbali na silaha hizo pia walikutwa na Radio “Call” mbili aina ya Kenwood zilizokuwa hewani na wimbi la Polisi Arusha, bullet proof moja, vifaa vya kusafishia bunduki, mifuko mitatu ya kubebea pesa na vifaa vingine.

Majambazi hao ambao kwa sasa miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru walikutwa pia na vitambulisho mbalimbali vya Jamhuri ya Kenya pamoja na simu tano aina ya Nokia, Tecno na Samsung. Kamanda Sabas alisema kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi juu ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwatafuta watuhumiwa wengine waliofanikiwa kukimbia na kubaini mtandao mzima wa kundi hilo.

Kamanda Sabas alimalizia kwa kuwashukuru wananchi wa Arusha kwa kushirikiana na Jeshi hilo juu ya utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu na kuonya yoyote ambaye atajiingiza katika matukio ya kufanya uhalifu Jeshi hilo litamkamata na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.


Pichani chini Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) akiwaonyesha waandishi wa habari silaha zilizokutwa toka kwa majambazi hao pamoja bullet proof huku picha ya mwisho waandishi wakishuhudia gari lililokuwa linatumiwa na majambazi hao.