Wakati tafiti za kienyeji zenye lengo la kupima kukubalika
kwa wagombea urais, hasa Dk John Magufuli na Edward Lowassa zikizidi
kuongezeka, polisi jijini hapa mwishoni mwa wiki walitumia nguvu kutawanya
vijana waliokuwa wakiendesha kura za maoni kwenye stendi ndogo ya mabasi na
soko kuu.
Tangu kutangazwa kwa matokeo ya utafiti uliofanywa na
taasisi za Twaweza na Ipsos, vijana kwenye maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko,
hasa sokoni na kwenye baa wamekuwa wakiendesha tafiti zao za kienyeji wakiwa na
lengo la kuonyesha hali halisi ilivyo mitaani tofauti na matokeo ya tafiti hizo
mbili.
Katika tafiti hizo za Ipsos na Twaweza, Dk Magufuli, ambaye
anagombea urais kwa tiketi ya CCM, alikuwa mbele ya Lowassa anayegombea kwa
tiketi ya Chadema na vyama vinavyounga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), lakini matokeo hayo yamepingwa vikali na wadau mbalimbali, huku yakiamsha
tafiti za kienyeji mitaani.
Katika tukio lililotokea mjini Arusha, vijana walikuwa
wakiendesha utafiti wao kwenye soko kuu la Arusha na eneo la kituo kidogo cha
mabasi, lakini polisi walifika na kuwatimua wakidai wanavunja sheria.
Wafanyabiashara hao wa soko hilo
na stendi ndogo, waliandaa maboksi mawili ya kura, moja likiwa limeandikwa
“Magufuli” na jingine “Lowassa”.
Baadaye walialika watu kwenda kupiga kura.
Kila aliyepita katika eneo hilo alielezwa utaratibu wa kupiga kura na
alitumbukiza karatasi yake katika boksi lililoandikwa jina la mgombea anayeona
anafaa kuwa rais.
Utafiti wa stendi ndogo ulikamilika baada ya muda na
ulionyesha matokeo ya wagombea hao (tunayo).
Wakati watu waliokuwa stendi ndogo wakiendelea kushangilia
matokeo hayo, wafanyabiashara wenzao wa soko kuu walikuwa wakiendelea kupiga
kura na ghafla polisi walipofika maeneo hayo na kuwatimua vijana waliokuwa
wakikusanya kura.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema
waliokuwa wanafanya utafiti huo walikiuka sheria na kwamba kitendo chao
kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuwa kulikuwa na watu
wasioafikiana.
Aliwataka wakazi wa Arusha kuacha kufanya mambo ambayo
hayana manufaa, badala yake wasubiri siku ya kupiga kura.
“Huo ni utafiti wa
aina gani wa maboksi?” alihoji alipoulizwa kuhusu tukio hilo .
“Hizi ni vurugu za
mitaani. Tunawaomba wananchi watulie, wasubiri siku ya uchaguzi wapige kura kwa
amani.”
Hili ni tukio la pili la utafiti unaofanywa kienyeji mitaani
baada ya wafanyabiashara wa Kariakoo, Dar
es Salaam kuendesha utafiti wao kwa kuruhusu watu
kumpigia kura mgombea wanayempenda kati ya Magufuli na Lowassa.
Mbali na utafiti huo wa wakazi wa Dar es
Salaam , kwenye maeneo mengine nchini kumekuwapo na watu
wanaoendesha tafiti kama hizo zenye lengo la
kujua ni mgombea gani wa urais anakubalika zaidi.
Wakati vijana hao wakifanya tafiti za kienyeji mitaani,
wadau mbalimbali wamekuwa na maoni tofauti kuhusu kushamiri kwa vitendo hivyo.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa na gazeti hili wamesema
kuanzishwa kwa tafiti hizo kunasadia kupata matokeo halisi ya joto la uchaguzi
katika maeneo husika, huku wataalamu wa tasnia hiyo wakieleza kuwa ni matokeo
ya kufeli kwa mfumo rasmi wa ufanyaji tafiti za kisayansi kutokana na misukumo
ya kisiasa.
Mkazi wa Tabata, Isaiah Salmon alisema kutokana na taasisi
zilizoaminiwa na wananchi kutofanya kinachotakiwa, yupo tayari kujitokeza
kushiriki tafiti za mitaani hata kama Serikali
inazikataza.
Alisema inasikitisha kuona mashirika makubwa kama Twaweza yanatoa matokeo ambayo hayaendani na hali
halisi katika mwenendo wa siasa nchini.
Salmon alisema anaona Dk Magufuli na Lowassa wanachuana
katika kampeni zinavyoendelea, lakini matokeo ya utafiti wa taasisi hizo ni
tofauti.
“Unakumbuka wakati wa
uchaguzi kule Kenya
tulikuwa tukipata matokeo ya tafiti zilizokuwa zikibainisha Uhuru Kenyatta na
Raila Odinga wanaachana kwa kiasi kidogo na ndivyo ilivyokuwa mitaani. Hata
matokeo ya uchaguzi yalivyotoka yalionyesha kama tafiti zilivyosema,”
alisema.
Pamoja na kuanza kushamiri kwa tafiti hizo, baadhi ya
wananchi wanatatizika na masuala ya kisheria na kanuni za uchaguzi na pia
kukosa imani na watu wanaoendesha tafiti hizo ambazo mara nyingi ni vijana wa
maeneo yenye watu wengi kama sokoni au stendi.
Mjasiriamali, Telesphory Ndomba alisema yupo tayari
kushiriki katika tafiti hizo, lakini hana uhakika na uhalali wa matokeo
yanayotolewa na watu wanaoweka maboksi hayo kama
ni kweli ya au yemetiwa chumvi.
“Tuna uhakika gani wale
wanaochukua hayo maoni watawasilisha inavyotakiwa? Mimi sijajua iwapo taratibu
na kanuni za uchaguzi zinaruhusu kufanya tafiti hizo za wananchi, lakini hata
nikiziona na nikashiriki bado siwezi kujua kama taratibu hizo zimefuatwa na
aliyetangazwa, kashinda kweli au la,” alisema.
Alisema pamoja na taasisi za kitafiti kuonekana zina
upungufu katika kazi zao, bado wana uhalali wao na kwamba tafiti za mitaani
zinafanyika kwa sababu wananchi wengi, akiwamo yeye, “wamechoshwa na ahadi hewa zisizotekelezeka hivyo wana hamu ya
kufanya mabadiliko”.
Hata wakati baadhi wanaona kushiriki utafiti huo unaozidi
kushamiri mtaani kama haki ya msingi, Emilia Masaka (29), alisema haoni kama kuna umuhimu wa kushiriki tafiti hizo.
“Binafsi utaratibu
huo mimi sina kwa sababu nina kazi zangu nyingi za kufanya kwa sasa. Sina
nafasi kabisa kushiriki hizo tafiti zao. Ila kama ningekuwa na nafasi
ningekwenda tu kuwaangalia ila siyo kushiriki,” alisema Masaka anayefanya
kazi katikati ya jiji.
Mtafiti kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Patience Mlowe alisema hatua ya wananchi kuanzisha kura zao maoni juu ya chama
au mgombea atakayeshinda urais, ni ishara tosha kuwa hawana imani na tafiti
zinazotolewa na mashirika mbalimbali wakati huu wa Uchaguzi Mkuu.
Mlowe alieleza kuwa tafiti nyingi zilizofanywa hivi karibuni
zinaonekana kuwa na msukumo wa kisiasa kwa kuwa watafiti walitumia muda mwingi
kuzielezea wakati kitaalamu inabidi mwananchi wa kawaida azielewe bila
kufafanuliwa au kuachwa na maswali lukuki yasiyo na majibu.
“Hayo ni matokeo ya
kuwa na tafiti zisizotoa hali halisi inayoendelea katika mchakato wa uchaguzi
na wananchi hawakupata matokeo halisi, ndiyo maana wameanzisha tafiti zao.
“Tafiti za aina hii
tuzitegemee tu katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuwa wananchi hawana imani
na tafiti zinazotolewa,” alisema Mlowe.
Alisema iwapo watu wanaoshirikishwa katika tafiti hizo za
wananchi ni wakazi wa maeneo husika na wana sifa za kupiga kura, hapana shaka
kuwa matokeo yanayopatikana yatasadifu hali halisi siku ya kupiga kura ambayo
ni Oktoba 25.
Pamoja na tafiti zinazofanywa na wananchi kutoonekana ni za
kitaalamu bado huenda zikaendelea kufanywa zaidi nchini kwa kuwa zinasadifu
hamu ya kupiga kura iliyopo miongoni mwa wananchi kama alivyoeleza, Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Damian Shumbusho.
“Huu utaratibu wa
wananchi kufanya tafiti zao kwa kupiga kura sokoni na vijiweni unaonyesha
bayana wananchi wamepata mwamko wa kushiriki uchaguzi. Wanaona siku ya uchaguzi
inacheleweshwa hivyo wanatafuta matokeo ya haraka haraka,” alisema
Shumbusho kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala.
Alisema tafiti za kupima kukubalika kwa vyama na wagombea
zinaweza kuwakatisha tamaa au kuwaongezea mori wapiga kura wakati huu wa
uchaguzi na hazitakiwi kutegemewa sana kwa kuwa muda zinaofanywa siyo sahihi na
siasa zinabadilika mara kwa mara.
“Kitendo cha wananchi
kusema hizo tafiti tupa kule ni sahihi kwa sababu zimechokoza wananchi walipopanga
kupiga kura baada ya kusikia sera za wagombea,” alisema.
Ofisa habari wa Twaweza, Risha Chande alisema kitendo cha
wananchi kufanya tafiti zao mitaani ni jambo jema kwa kuwa kinaonyesha wana
hamu ya kushiriki katika tafiti mbalimbali za kitakwimu jambo ambalo halikuwapo
hapo awali.
Chande alisema pamoja na wananchi hao kuonyesha hamasa ya
maswala ya kitakwimu bado, methodolojia wanazotumia haziwezi kutoa matokeo
halisi ukilinganisha na tafiti za kisayansi zinazohusisha uchaguzi makini wa
sampuli za kutafiti.
“Lazima tufuate
utamaduni wa kuangalia au kujihakikishia mambo hasa maswala ya kitakwimu na hilo ni jambo letu kama
taasisi.
“Sasa kama ukiwa na
ugomvi na kitu lazima utachukua hatua kama waliyofanya wananchi hao ila
tutambue kuwa kuna tofauti nyingi baina ya utafiti wao na ule wa kwetu,”
alisema.