Inawezekana mara kwa mara umekuwa ukiwaza namna unavyoweza kuanzisha
biashara yako na kujenga uhuru wa kifedha. Mawazo hayo umekuwa ukiyapata hasa
kutokana na kila ukiangalia unaona kama vile
kipato chako hakitoshi kutokana na kazi unayoifanya sasa. Kama
hayo ndiyo mawazo yako upo kwenye njia sahihi.
Nikiwa na maana kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuanzisha
biashara yako mwenyewe kuliko hata unavyofikiri. Kwani mbali na faida ya
kifedha yapo mambo mengine mengi utakayojifunza kutokana na kumiliki biashara
yako mwenyewe. Je, unajua ni kwa sababu gani unatakiwa kumiliki biashara yako
mwenyewe na kuacha kutegemea kuajiriwa kwa asilimia zote ?
Hizi Ndizo Sababu 8 Kwanini Unatakiwa Kumiliki Biashara
Yako Sasa?
1. Ni njia bora ya
kukufikisha kwenye uhuru wa fedha.
Inawezekana ukawa umechoka na kazi unayoifanya na unaoina
haifai kwa namna moja au nyingine. Lakini njia bora ya kuweza kuondokana na
utumwa huo ambao unakukabili ni kuanzisha biashara yako mwenyewe ambayo
utaisimamia mpaka ikuletee mafanikio unayoyahitaji.
2. Ni Njia bora ya
kujifunza.
Hakuna njia bora ya kujifunza kuhusu kutunza na kumiliki
pesa kama biashara. Hili ndilo eneo ambalo utajifunza mengi kuhusu masoko, namna
ya kukuza mtaji na jinsi ambavyo unaweza ukaufikia uhuru wa kipesa. Kwa hiyo kama una biashara yako inakusaidia kujifunza yote hayo
hatua kwa hatua.
3. Ni njia bora
yakujifunza kujitegemea.
Unapokuwa kwenye ajira kwa kawaida unakuwa unamtegemea mtu
fulani ambaye ndiye akuamulie juu ya maisha yako. Lakini kwenye biashara mambo
hayako hivyo. Wewe ndiye unakuwa mwamuzi mkubwa wa maisha yako. Na unakuwa
unakikisha unafanya kila linalowezeka mpaka biashara yako ifanikiwe.
4. Inakuwa inakupa
hamasa ya mafanikio zaidi.
Huo ndiyo ukweli unaotakiwa ujue kuwa, unapokuwa na biashara
inakuwa inakupa hamasa ya kuweza kufanikiwa na kusonga mbele zaidi. Tofauti na
ajira ni rahisi kusema kuwa ‘aaah kazi yenyewe siyo yangu kwanza’ kwa hiyo
unakuwa unafanya kwa jinsi unavyojisikia. Lakini kwenye biashara mambo hayako
hivyo ni lazima kujituma ili kufanikiwa.
5. Inakuongezea
ujasiri.
Unapokuwa mfanyabishara ni hatua nzuri sana kwako ya kukupelekea kuwa na ujasiri wa
hali ya juu. Hiyo yote ni kwa sababu unapofanikiwa katika biashara moja unakuwa
ndani yako una hamasa kubwa ya kutaka kufanya biashara nyingine tena kwa
mafanikio. Kwa hali hiyo unakuwa una maamuzi mengi ya kijasiri ambayo ni rahisi
kukusaidia kukusonga mbele.
6. Ni njia rahisi ya
kufuata mipango na malengo yako.
Mara unapoanzisha biashara yako unakuwa upo kwenye njia
sahihi ya kufuata ndoto za maisha yako. Hii yote ni kwa sababu unakuwa
unakifanya kile kitu ambacho unakipenda kwa dhati toka moyoni mwako. Wakati
unapokuwa kwenye ajira unakuwa unafanya tu ilimradi mkono uende kinywani. Hiyo
ndiyo faida kubwa mojawapo ya kuwa kwenye biashara.
7. Inakufanya unakuwa
ni mtu wa vitendo.
Watu wengi mara nyingi ni waongeaji bila ya kuwa watu wa
vitendo. Lakini kitendo cha kuwa na biashara yako mwenyewe inakupelekea unakuwa
ni mtu wa vitendo. Utaelewa vizuri umuhimu wa kuchukua hatua katika biashara
tofauti na ambavyo ungekuwa hufanyi biashara ingekupelekea wewe kuwa na maneno
mengi bila utekelezaji.
8. Ni njia bora ya
kufanya mambo mengine zaidi.
Unapokuwa kwenye biashara inakuwa ni njia bora ya kufanya
mambo mengine bora zaidi. Kama ulikuwa una
lengo moja na umelikamilisha inakuwa ni rahisi kuweza kulifatilia lengo lingine
mpaka tena kulifanikisha. Na hiyo nguvu yote ya kufanya mambo mengine inakuja
kutokana na ujasiri ambao tayari unakuwa umeshajijengea kwenye biashara yako.