TUME ya Taifa ya Uchaguzi inayotarajiwa kusimamia uchaguzi
mkuu, Oktoba 25 mwaka huu, imetangaza rasmi siku ya uchaguzi wa majimbo ya
Lushoto na Ulanga Mashariki kufuatiwa na vifo vya wagombea wa majimbo hayo.
Akizungumza na wanahabari kwenye ukumbi wa New Africa Hotel jijini Dar es Salaam leo wakati wa
mazungumzo na wawakilishi wa watu wenye ulemavu, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva, amesema kuwa tume imepokea taarifa za vifo vya
wagombea wa ubunge majimbo ya Lushoto (CHADEMA) na Ulanga Mashariki (CCM).
Amesema kuwa mbali na wagombea hao wa ubunge pia kuna
wagombea wanne wa udiwani katika kata za Bomang’ombe-Wilaya ya Hai (CCM),
Bukene-Shinyanga (CCM) Msingi-Mkalama Singida (CHADEMA) Muleba (CCM) Uyole
–Mbeya (CCM) ambao wamefariki, hivyo chaguzi hizo kuahirishwa hadi tarehe
aliyoitaja.
Alisema kwa kufuata sheria na taratibu za tume hiyo, imeona
vema mchakato wa uchaguzi kwa majimbo hayo upande wa uteuzi wa wagombea
ufanyike Oktoba 12 mwaka huu .
Aidha Lubuva alisema kampeni zitaanza mara baada ya uteuzi
wa wagombea wa wabunge na madiwani Oktoba13 hadi Novemba 18 huku uchaguzi
ukifanyika Novemba 22 mwaka huu.
Kwa upande wa watu wenye mahitaji maalum kama walemavu
alisema kuwa tume tayari imejipanga kuhakikisha kwamba watu walemavu wanapata
msaada pindi wawapo kwenye vituo vya kupigia kura, hivyo kwa kuzingatia hilo
tume imetoa maelekezo kwa wasimamizi wa vituo na namna ya kuwahudumia mara
watakapo fika katika vituo vya kupigia kura ili wapewe kipaumbele.
Vilevile aliongeza kuwa upande wa watu wenye ulemavu wa
kutoona tume imeandaa kifaa kijulikanazo kama “Tactile Ballot Folder”
kitakachowasaidia kupiga kura pasipo kusaidiwa na mtu yeyote na hivyo kutimiza
lengo la usiri wa kura ya mpiga kura.