Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema utafiti kilioufanya tangu
kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unaonesha kuwa mgombea urais
wa Zanzibar kwa
tiketi ya chama hicho, Dk Ali Mohamed Shein anaongoza kwa zaidi ya asilimia 60
dhidi ya wagombea wa vyama vingine.
Akizungumza kwenye ofisi za chama hicho zilizopo Kisiwa Ndui
leo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai amesema matokeo hayo yametokana na
kazi nzuri aliyoifanya Dk Shein katika miaka mitano ya awamu ya kwanza ya
uongozi wake.
“Tathmini imeonyesha
kuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM anakubalika zaidi kuliko wagombea
wote wanaoshiriki kwenye uchaguzi huu na kwa kukisia tayari anaongoza kwa zaidi
ya asilimia 60,” amesema Vuai
Ameongeza kuwa tathmini hiyo inaonyesha kuwa Dk Shein anaongoza
kutokana na udhaifu wa mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad anayegombea
kwa mara ya tano bila mafanikio.
Vuai amesema kuwa Dk Shein amewapiku wagombea wengine
kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya
chama hicho kwa asilimia kubwa.
Tathmini hiyo inaonyesha kuwa CCM inatarajia kupata kura
nyingi kutoka Pemba ambako kwa muda mrefu
kumekuwa ni ngome ya CUF.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM ameeleza kuwa wana CCM katika
kisiwa hicho wamekua kidemokrasia hivyo uchaguzi huu hawatatishwa kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizotangulia.