Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan)
imetoa tuzo kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kuwa taasisi bora ya
serikali nchini kwa kutoa taarifa kwa wananchi, huku Wizara ya Ushirikiano wa
Afrika Mashariki inayoongozwa na Waziri Dk. Harrison Mwakyembe ikiongoza kwa
urasimu wa kutotoa taarifa kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Misa-Tan, Simon Berege aliyasema hayo jana
jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utafiti uliofanywa kwa ajili ya
kuangalia taasisi za umma namna zinavyotoa taarifa kwa wananchi.
Alisema lengo la utafiti huo ni kuhakikisha uhuru wa habari
unatambulika ndani ya Katiba kama haki ya
msingi pamoja na kuhamasisha uwazi na uwajibikaji.
Berege alisema lengo jingine la utafiti huo ni kuangalia
jinsi gani wananchi wa kawaida wanaweza kupata taarifa muhimu katika taasisi za
umma ambazo zinawasaidia kufanya maamuzi sahihi katika maisha yao .
Utafiti huo ambao Juni mwaka huu ulihusisha idara nane za
serikali na kati ya hizo mbili zilishiriki mwaka jana.
Alizitaja taasisi za umma zilizofanyiwa utafiti huo kuwa ni
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Wizara ya
Maliasili na Utalii, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wizara ya Ardhi na
Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Katika utafiti huo, Berege alisema waliwatumia wananchi wa
kawaida ambao waliandika barua ama kufika katika taasisi hizo kutaka taarifa
mbalimbali na baada ya kufanya hivyo walisubiri kuona ni nani anayejibu kwa
haraka.